HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 24, 2013

Benki ya Azania yapiga tafu ujenzi wa bwalo la chakula shule ya sekondari Mahege

 Ofisa Maendeleo ya Biashara , Benki ya Azania, Othman Jibrea (kushoto) akikabidhi hundi ya shilingi milioni kumi kwa Faulu Maeda (kulia) Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mahege iliyopo wilaya ya Rufiji ikiwa ni mchango wa benki hiyo kusaidia ujenzi wa bwalo la chakula la shule hiyo. (Na Mpiga Picha Wetu)
Afisa Maendeleo ya Biashara , Benki ya Azania, Othman Jibrea (kushoto) akikabidhi mfano wa hundi kwa Faulu Maeda (kulia) Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mahege iliyopo wilaya ya Rufiji ikiwa ni mchango wa benki hiyo kusaidia ujenzi wa bwalo la chakula la shule hiyo.


Na Mwandishi Wetu

BENKI ya Azania imekabidhi shilingi milioni kumi kwa Shule ya Sekondari ya Mahege iliyopo katika wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani ambazo zitasaidia kuendeleza ujenzi wa bwalo la chakula la shule hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika shuleni hapo katika kijiji cha Mahege mwishoni mwa wiki, Afisa Maendeleo ya Biashara , Benki ya Azania, Othman Jibrea alisema kuwa benki yake imejikita katika kusaidia maendeleo ya shuguli mbali mbali za kijamii .  

Jibrea alisema kuwa mchango wa benki yake kwa shule hiyo utasaidia kuboresha mazingira ya kuishi na kujisomea katika shule hiyo.

“Ni utamaduni  wa Benki ya Azania kutoa michango mbalimbali kwa jamii sambamba na mpango wetu wa kusaidia jamii katika shughuli mbalimbali. Tunafahamu shida wanayoipata wanafunzi wakati wa chakula kwa sababu ya kutokuwepo kwa bwalo la chakula shuleni.

“Benki ya Azania leo inachangia shilingi milioni kumi zitakazosaidia katika mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula la shule. Tunaamini mchango wetu utasaidia kuboresha mazingira ya shule ya kujisomea,” alisema Jibrea.
Alisema kuwa benki yake itaendelea kusaidia miradi  mbalimbali ya maendeleo ya kijamii nchi nzima katika sekta mbalimbali ikiwa ni  elimu na afya. 

“Benki ya Azania imesaidia miradi mbalimbali katika sekta mbali mbali hasa za afya na elimu. Mwaka huu tumesha changia kampeni dhidi ya saratani ya matiti na tutaendelea kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii za maendeleo ,” alisema Jibrea.

Awali Mkuu wa Shule ya Mahege, Faulu Maeda wakati wa hafla hiyo alisema kuwa shule bado inahitaji msaada wa kifedha ili kukamilisha ujenzi wa mradi huo na kutoa wito kwa makampuni mengine na watu binafsi kujitokeza kuisadia shule hiyo.

“Tunashukuru kwa mchango uliotolewa na Benki ya Azania. Kumalizika kwa mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula la Mehege bado ni safari ndefu. Tunatoa wito kwa makampuni mengine kutusaidia aidha kwa kutoa vifaa vya ujenzi au fedha ili tuweze kumalizia mradi,” alisema Maeda.

No comments:

Post a Comment

Pages