HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 24, 2013

MANCHESTER CITY, CHELSEA VITANI ETIHAD LEO


LONDON, England

“Tunapaswa kupigana kuhakikisha tunashinda ili kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa. Pointi 12 nyuma ya vinara Man United ni nyingi, lakini zitakuwa mzigo zaidi kwetu kama zitaongezekla na kufikia 15 kwa kufungwa na Chelsea”

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City, leo inashuka dimba la nyumbani la Etihad kuwaalika Chelsea – katika mechi kali iliyobeba hatima ya City katika jaribio la kutetea taji hilo ililotwaa baada ya kulisaka kwa miaka 40.

Kocha Roberto Mancini amekiri hatima ya kikosi chake iko mikononi mwao wenyewe na kuongeza kama watakubali kuchapwa nyumbani na The Blues, hawatakuwa na ujanja tena wa kuikamata Manchester United.

“Tunapaswa kupigana kuhakikisha tunashinda ili kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa. Pointi 12 nyuma ya vinara Man United ni nyingi, lakini zitakuwa mzigo zaidi kwetu kama zitaongezekla na kufikia 15 kwa kufungwa na Chelsea,” alisema Mancini.

Matumaini ya Mancini yako katika mechi baina ya kikosi chake na Man United, ambapo aliongeza: “Lazima tuwe na matumaini kwamba Man United inaweza kupoteza pointi kati ya sasa na pambano letu la mahasimu ‘Manchester Derby’.

“Hiyo ndio pekee itakayotupatia nafasi ya kupigania ushindi wetu. Mpaka sasa hautujui kama tutamaliza tukiwa nafasi ya kwanza, ya pili au ya tatu. Tuna mechi 12 zimesalia, ni lazima tucheze kwa kiwango chetu cha juu hadi mwisho wa msim.

“Kisha mwishoni mwa msimu tutaona waoi tutakapokuwa na kipi kitatokea juu yetu. Kama utaniuliza kuwa nitafurahi kumaliza ligi nikiwa nafasi ya pili, nitakwambia hapana, itanisikitisha sana.”

Man City iko nafasi ya pili ya msimamo, ikiwa na pointi 53, huku United ikiongoza kwa pointi 65 kabla ya mechi za jana na leo. Chelsea wako nafasi ya tatu wakiwa na pointi 49 na wanaweza kupanua wigo wa pointi kama wataifunga City, ingawa itasalia katika nafasi hiyo hiyo.

Man City inaingia dimbani ikijivunia rekodi ya jumla ya kuichapa Chelsea mara 61 katika mechi zao 146 walizokutana, huku Chelsea ikishinda 47 na kutoka sare mara 38.

Mara ya mwisho miamba hii kuumana ilikuwa ni Novemba 25, 2012 kwenye dimba la Stamford Bridge jijini London, ambapo walitoka sare ya 0-0, katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi hii.

Wakati Man City ikiialika Chelsea Etihad, Newcastle United watakuwa nyumbani St James Park kuwakaribisha Southampton – katika mechi nyingine ya Ligi Kuu leo Jumapili.

BBC

No comments:

Post a Comment

Pages