Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Exim, Dinesh Arora
(katikati) akimfanyia usaili Faraji Mussa (kulia) mwanafunzi wa mwaka wa tatu
katika kitivo cha Uchumi na Takwimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
wakati wa maonyesho ya Career Day Fair yaliyofanyika chuoni hapo mwishoni mwa
wiki. Kushoto ni Meneja Msaidizi Rasilimali Watu wa Benki ya Exim, Hetal
Ramaiya. (Na Mpiga Picha Wetu)
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Exim
imetangaza mpango wa kutoa nafasi za ajira zaidi kwa wahitimu kutoka vyuo vikuu
mbalimbali nchini ikiwa ni mpango wa benki hiyo wa kukuza sekta ya ajira.
Akizungumza katika maonyesho
ya vyuo vikuu maarufu kama Career Day Fair yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Exim, Dinesh Arora
alisema kuwa vyuo vikuu vina nafasi kubwa ya kuziba pengo la upungufu wa wafanyakazi
katika sekta ya kibenki na fedha nchini.
“Baada ya uanzishwaji
wa kituo chetu cha mafunzo kinachojulikana kama Exim Academy, benki yetu sasa
imeamua kuwalenga wahitimu moja kwa moja kutoka vyuoni na uzoefu hautakuwa
kipingamizi kutokana na kuwa wahitimu hao watapatiwa mafunzo muhimu pindi watakapojiunga
na benki yetu.
“Nimebahatika kufanya
usaili kwa baadhi ya wahitimu leo na nimeona wengi wana uwezo mkubwa sana. Baada
ya zoezi hili kukamilika, Tutachagua baadhi yao ili wajiunge na benki,” alisema
Arora.
Awali, Meneja
Mwandamizi wa Tawi la Benki ya Exim la Clock Tower, Agnes Kaganda aliwapa
changamoto wahitimu hao kuwa makini katika maisha ili kufikia malengo na ndoto
zao.
“Katika hii dunia
hakuna kisichowezekana. Naomba mwendelee kufanya kazi yoyote itakayopatikana
bila kukata tamaa na usiruhusu mtu yoyote kukuvurugia ndoto zako.
Kwa upande wake makamu
wa rais wa Kamati ya Mandalizi ya maonyesho hayo, Wendo Lendo alisema kuwa
maonyesho hayo yametoa fursa kwa wahitimu hao kujuana na makampuni mbalimbali
makubwa.
“Maonyesho ya leo
yameonyesha mafanikio kwa kuwa mfumo wa elimu wa Tanzania hausaidii katika
kuwajengea uwezo wahitimu wa kuajiriwa. Zaidi ya makampuni 20 yameshiriki leo
hii na ninauhakika kwa mwaka ujao maonyesho yatakuwa makubwa na yenye mafanikio
zaidi,” alisema Lwendo.
No comments:
Post a Comment