HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 22, 2013

Jaji Kaganda Umemung’unya Maneno


“Zimwi likujualo halikuli likakuisha”
 
Na Bryceson Mathias
 
KAMA Mwananchi wa Kawaida, napata tabu,  na sijui walalahoi wanaonaje ikiwa watu wa kutegemewa kama Jaji Mstaafu Tume ya Maadili, Salome Kaganda, anaweza akaadibu Wabunge wanaokithiri kutukana matusi bungeni halafu isiwataje Majina yao, Majimbo na Vyama vyao ili kuwaonya, wasirudie tena.
 
Sikubaliani na kubebana kwa namna hiyo, kwa sababu kwa kufanya hivyo ndiko kunawafanya wabunge  wa namna hiyo waonekane wanatoboa mbereko ya Tanzania kana kwamba walitumwa kufanya hivyo, na walichofanya kinakubalika na vyombo vyote vya maadili ikiwemo Serikali.
 
Kama hayakubarikiwa, basi tungeona Jaji Kaganda na Timu yake wanawaita Wabunge hao na kuwapa Kiti Moto   pamoja na kuwakanya na kuwakalisha Kikao wao na Viongozi wao Kitaifa Vyama na Serikali, ili kuwaadabisha kutokana na kile walichofanya bungeni, maana kinachafua heshima ya Taifa, ambapo tusipofanya, vitarithiwa.
 
Kwa upande mwingine, Semina ya wabunge kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni Dodoma hivi karibuni, itakuwa haina maana ikiwa Jaji Kaganda na Tume yake hawatawaita na kuwahoji wabunge hao sababu za kutoa matusi kwenye Kiunga cha Kimataifa.
 
Nasema Tume hiyo ifanye hivyo kwa sababu, jambo walilofanya ni mbegu iliyopandwa kwenye Udongo wenye rutuba, na sasa inaoza, itamea, litamwagiliwa, litapaliliwa, litaiva na baadaye itakomaa kwa kizazi hiki na kijacho, na kuwa Jambo la kawaida.
 
Hivi karibuni tumekuwa tukilalamika kuwa maadili nchini yanaporomoka lakini wabunge wa kutegemewa ndio wanakuwa wa kwanza kuporomosha matusi, na kama hatutayafuta matamko hayo kwa kuwaadabisha wakengeufu miongoni mwetu. Ipo siku makaburi ya watu fulanifulani siku za usoni yatatandikwa viboko.
 
Mimi nilitegemea Jaji Kaganda atamwambia na kumkosoa kila Mbunge aliyetukana matusi, akianzia na Naibu Spika Job Ndugai, ambaye akikaa kwenye Kiti huwa anajisahau, asitambue kuwa ni Mtu mwenye dhamana kubwa, lakini utaona anaanza Utani akiwa kwenye kiti cha heshima, na utani huo baadaye hupelekea Vurugu.
 
Nilijua Jaji Kaganda atamuonya Mbunge wa Mtera (CCM), ambaye licha kutukana Wabunge wenzie kuwa wana Mimba Isiyotarajiwa, amekuwa na historia ya kutukana Matusi hata kwenye Kampeni za Chaguzi mbalimbali, mfano Ameru; ambapo sasa sidhani kama watanzania hadi leo wanamstahi kama Mhe.
 
Nilikusudia, Kaganda amkemee Mwandishi na Mtangazaji Mkongwa wa habari, na Mbunge wa Jimbo la Kondoa Kusini Juma Nkamia(CCM), kwamba kitendo alichofanya kinaidharirisha Taaluma ya Habari, mbali ya kumpunguzia Heshima na umaarufu wake  Kitaifa na Kimataifa dhidi ya Taaluma yake Nyeti.
 
Kaganda angeweza kumsaidia Mbunge Khatibu Said Haji (Konde - CUF) ambaye alitoa matusi ya Nguoni ambayo kimsingi kwa wadhifa wake hakutakiwa atoe kinywani mwake; na Mbunge wa Magomeni Mohamed Amour Chombo, aliyemwaga matusi ya Nguoni pia, bila wao kutukanwa.
 
Ningependa nione Kaganda akiwaeleza ufasaha wa kosa walilokosea, Peter Msigwa –Iringa (CHADEMA), Joseph Mbilinyi (Sugu) Mbeya, na Ezekiel Wenje kutokana na Makosa yao ili kuadibu kila upande wa Shilingi kwa faida ya Watanzania na kizazi kijacho.
 
Aidha ningekuwa Rais na Kiongozi Mkuu wa Bunge la Tanzania, ningeliliambia Taifa toba, jinsi nisivyoafikiana na Matusi yaliyofanywa na wabunge kwa ujumla wao,  ningejisafisha na kukataa kwamba siyabariki hayo, na kwa sababu wote wamechaguliwa na wananchi, wao wana jambo la kuwafanya, kama wanawafaa
 
 
0715933308. 

No comments:

Post a Comment

Pages