HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 14, 2013

Mwakyembe–Utagawana Maumivu na Mwenye Njaa?


‘Usiache Mbachao kwa Msala upitao!’
Bryceson Mathias
WAKATI wa wananchi wengine wanaishi kwa kula mizizi, wadudu jamii ya kumbikumbi,  Senene, na Mboga, Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe aliwataka Wananchi wakubali kugawana Maumivu na Wasafirishaji kuhusu ongezeko la Nauli nchini.

Akizungumza na wandishi wa Habari mjini Dodoma, Dk. Mwakyembe alisema, Serikali iliridhishwa na Kauli ya SUMATRA kutaka bei hizo ziongezwe ingawa alilalamikia wananchi kulalama bila kuhudhuria vikao vya maridhiano ili penye maumivu wakate rufaa au kupinga.

Dk. Mwakyembe; wewe ni Mwanasheria, Kabla sitajatoa msimamo wangu niulize swali, uliwahi kuona wapi Kesi ya Tumbili Mahindi, akahukumu Nyani na Mkulima akapewa Haki? Hivi Mlala Hoi wa Kyela ‘Interior’ anaweza kupingana au kukata Rufaa kwa mtu mwenye Pesa akashinda?

Kabla ya kuridhia Nauli zilizotangazwa na SUMATRA nchini kote, Dk. Mwakyembe alisema Serikali iliihoji Sumatra na Baraza la Watumiaji Huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka hiyo kwamba taratibu zote zilizingatiwa.

Dk. Mwakyembe; Hivi kujua maumivu na adha ya Ongezeko la Nauli anaulizwa Sumatra na Baraza hilo! au wananchi wanaohudumiwa na ambao ndio wenye Serikali yao? Wananchi hawakumchagua Sumatra kuwa Kiongozi wan chi ila waliichagua Serikali yao inayowajika kwao.

Kufanya hivyo ni sawa na kuwauliza Askari wa Kiyahudi Yesu asuluniwe au asisulubiwe ni lazima watajibu asulubiwe kwa sababu alikuwa anahatarisha Utawala na Mafanikio ya Pilato na Farao katika nchi ya Uyahudi.

Hivyo kwa uhusiano wa maslahi uliopo kati ya SUMATRA, Baraza na Wasafirishaji, nisingetegemea SUMATRA iulizwe kama imefanya taratibu sahihi au haikufanya kwa vyovyote lazima itatetea kwa sababu kuna mgongano wa kimaslahi.

Kwa maisha ya magumu, shida na Njaa ya chakula iliyopo nchini, sikutegemea iwapo Serikali kupitia kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe, ingefikia mahali pa kuwamalizia wananchi kipato kidodogo walichonacho, ili wakidhi mfumuko wa bei na ugumu wa maisha walionao.

Ni kweli waswahili husema usiache mbachao kwa msala upitao; Je waziri Mwakyembe umsahau kuwa wananchi wako hivi karibuni waliathiriwa na Mafuriko huko mbeya. Je wakiongezewa Nauli kiasi hicho, watawezaje kumudu kufikisha bidhaa za muhimu katika maeneo yao?

Aliyeshiba hamjui mwenye Njaa; nilichoona Waziri amewauliza na kupata mawazo kwa watu ambao tayari walishashiba, hivyo kwao kuelewa adha na machungu ya Njaa na ukulima hawajui, wanachojua ni mahesabu ya kubuni gharama hata kama hazifiki hapo.

Kimsingi ninachoona, kumefanyika upendeleo kwa wenye umiliki wa usafiri, na pia SUMATRA na Baraza, wametumika kama vyombo vya kuwabeba kurahisisha (Cartelists) wa madai yao kukubalika, lakini wananchi wanaumia.

Naseme tena kwa kurudia na Msisitizo kwa Waziri wa Uchukuzi Dk. Mwakyembe kwamba, kimsingi mtu mwenye nacho hawezi kugawana maumivu na Mwenye Njaa, yaani asiyenacho (Mlalahoi) kwa vyovyote kila siku atamdhulumu?

Nakukumbusha Tena Dk. Mwakyembe, huu ni wakati wa kuwasaidia wanyonge Ijabu tu hata uchovye tone la Maji liwaburudishe walala hoi kwenye makoo yao, maana hakika wamepigika na kinachoitwa uwekezaji na mikataba mingi ya siri inayowaburuza wananchi katika haki yao.

Aidha nakukumbusha; Yesu alirudi mara ya pili kwa Lazaro, safari hii ilikuwa kumuimarisha na kuzungumza naye kama rafiki yake Mkuu. Naomba usipoteze wasifu wako kwa wasiokuwa nacho, wanakutegemea uwatetee. Dk. Mwakyembe, Ukila na kipofu usimshike mkono.

0715933308

No comments:

Post a Comment

Pages