Na Mwandishi wetu
MKURUGENZI Mkuu wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Profesa John Nkoma, amewataka watumiaji
wa simu za mkononi kuhakikisha wanazisajili zimu zao kabla ya Julai 10 mwaka
huu kinyume chake zitafungwa.
Taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na
Mkurugenzi huyo, ilisema, pia Juni Mosi mwaka huu saa sita usiku laini zote za
simu ambazo hazijaanza kutumika zitafungwa na hazitaruhusiwa kutumika hadi
mtumiaji atakapoisajili laini yake mpya na watoa huduma husika.
Profesa Nkoma alisema watumiaji wa simu hizo na wananchi
wanashauriwa kuunga mkono juhudi zinazofanyika ili kufanikisha usajili huo wa
namba za simu kwa ajili ya kudumisha na kuendeleza amani, usalama na
kuharakisha maendeleo ya sekta ya mawasiliano na Taifa kwa ujumla.
Alisema ili kusajili namba hizo mtumiaji anapaswa kwenda kwa
mtoa huduma wake au wakala akiwa na kitambulisho chenye picha yake, kutoa
taarifa sahihi.
Profesa Nkoma alisema Sheria ya mawasiliano ya kielektroniki
na Posta (EPOCA), ya mwaka 2010, kifungu cha 131, kimeainisha kuwa ni kosa la
jinai kutumia au kuwezesha kutumika namba ya simu isiyosajiliwa.
Aliongeza kuwa adhabu ya kosa hilo ni faini ya sh 500,000 au
kifungu cha miezi mitatu ambayo itatolewa kwa yeyote atakayekiuka sheria hiyo.
Aidha, iwapo umesajili simu yako, mamlaka inakushauri
kuthibitisha usajili huo kwa kupiga *106#, kama wewe ni mtumiaji wa huduma
zilizoko kwenye mfumo wa GSM (Vodacom, Airtel, MIC (Tigo) na Zantel), kwa
wateja wanaotumia huduma za mfumo wa CDMA (Biol, SASATEL, TCCL Mobile na Zantel
Data), watapiga namba 106 ambapo watasikiliiza maelekezo.
“Taarifa utakayoipata inatakiwa kutaja jina lako kama
mtumiaji halali wa namba husika, na iwapo utapata jibu tofauti, tafadhali fika
kwenye ofisi ya mtoa huduma wako au wakala wake ili kurekebisha kasoro
hizo”alisema Profesa Nkoma.
No comments:
Post a Comment