DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE,
THE
STATE HOUSE,
P.O. BOX
9120,
DAR
ES SALAAM.
Tanzania.
|
Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Mheshimiwa Profesa Ibrahim
Lipumba amekaririwa na Gazeti la Mwananchi la leo, Jumatano, Mei 15, 2013
akisema kuwa “amenasa taarifa za siri za kuwepo kwa mipango ya kuongeza muda
wa Serikali ya sasa kukaa madarakani”.
Katika habari hiyo iliyoandikwa chini ya kichwa cha
habari, “Lipumba: Kuna njama za kumwongezea JK muda” Mheshimiwa Lipumba
anadai kuwa Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete “ itakaa madarakani hadi mwaka 2017” kwa sababu kuna “wasiwasi kuwa mchakato wa
sasa wa kupata Katiba Mpya hautaweza kukamilika mwaka 2014.”
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda
kufafanua kuwa taarifa hiyo ya Mheshimiwa Prof. Lipumba ni uzushi mtupu na ni upotoshaji
usiokuwa na msingi. Rais Kikwete
hafahamu kuwepo mipango hiyo. Ni vyema
Mheshimiwa Lipumba aisaidie jamii kusema nani anafanya mpango huo ili ukweli
ujulikane. Aidha, Mheshimiwa Rais
anawasihi wanasiasa na Watanzania kwa ujumla kuacha tabia za uongo na uzushi na
kuwapotezea muda Watanzania kufikiria mambo yasiyokuwepo.
Ukweli ni kwamba, kama ambavyo amesema mara nyingi, ni
matarajio ya Rais Kikwete kuwa mchakato wa Katiba utakamilika mwaka 2014 na
kuwezesha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kufanyika chini ya Katiba Mpya kama
inavyotarajiwa na kumpa nafasi ya kustaafu mwisho wa kipindi chake cha uongozi
wa taifa letu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
15 Mei, 2013
No comments:
Post a Comment