Mwenyekiti wa Yanga Lawrance Mwalusako, akimtambulisha mshambuliaji Mrisho Ngassa jana katika Makao Makuu ya klbu hiyo makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani Dar es Salaam.
DAR ES SALAAM, Tanzania
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limegeuka bubu na
kushindwa kuzungumzia kwa kina sakata la usajili wa mshambuliaji Mrisho Ngasa,
aliyetua Yanga akitokea Simba inayodai kuwa na mkataba naye wa mwaka mmoja wa
kuichezea.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, jana alizungumza na
wanahabari, huku akishindwa kuyatolea tamko madai ya Wekundu wa Msimbazi kuwa
mahasimu wao Yanga wametumia ‘njia haramu’ kupata saini ya nyota huyo wa zamani
wa Azam.
"Yanga imeripoti kumsajili Ngasa, huku Simba ikidai ni
mchezaji wake. TFF katika hili ingependa kujiweka mbali kwa sasa, hadi wakati
muafaka utakapofika litazungumza nani yuko sahihi kwa mujibu wa vielelezo
tulivyonavyo mikononi," alisema Wambura.
Alisisitiza kuwa, TFF inaheshimu mchakato uliofanyika hadi
sasa na haipendi kujiingiza katika hilo, ingawa itafuatilia vielezo vyake kuona
kama anastahili kusajiliwa Yanga na kama Simba ingali na mkataba naye kisha
kutoa tamko rasmi.
Aliongeza kuwa, mkataba halali wa mchezaji yeyote ni ule
uliowasilishwa mikononi mwa TFF na kwamba italiamua jambo hilo kwa kuzingatia
sheria na kanuni hiyo na hakuna atakayenyimwa haki yake katika maamuzi husika.
Akizungumza juzi baada ya Yanga kumtambulisha Ngasa,
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspop, alisema kuwa Ngasa
ni mchezaji wao halali na Yanga itawalazimu kuketi mezani na klabu yake ili kumnunua.
Hanspop alisema kuwa, mkataba wa Ngasa ulioisha ni ule wa
mkopo kutoka Azam kwenda Simba, ambayo alifanya nyongeza ya mkataba wa mwaka
mmoja unaoanza pale unapoishia mkataba wa mkopo ambapo ni hivi sasa.
"Yanga wamezoea ‘usajili haramu’, wakitegemea kubebwa kama
ilivyo kawaida yao. Mkataba wetu na Ngasa uko wazi, ulioisha ni ule wa mkopo kutoka Azam, bado ule wa mwaka mmoja aliosaini nasi.
"Kama wanamuhitaji ni
suala wao kutufuata kisha kukubaliana dau la kumsajili na sio kukurupuka kama
walivyofanya," alisema Hanspop.
No comments:
Post a Comment