Serikali
Mkoa Shinyanga imeondoa baadhi ya michango inayotozwa katika shule za Sekondari
ambayo imekuwa kero na mzigo kwa wazazi, hasa mwanafunzi anapoanza kidato cha
kwanza.
Maamuzi hayo
yamefikiwa katika kikao cha Wadau wa Elimu kilichofanyika jana chini ya
Mwenyekiti wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Ally Nasoro Rufunga
ambacho kiliwahusisha wadau mbalimbali wa Elimu ndani ya Mkoa kuanzia
wanafunzi, wazazi, walimu,viongozi wa serikali,wataalamu wa Elimu na viongozi
wa vyama vya siasa,asasi za serikali na binafsi.
Michango
hiyo imeondolewa baada ya wazazi wengi kutoa malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa kuwa,
kumekuwa na michango mingi mbali na karo, ambayo wazazi wanashindwa kumudu
gharama hivyo kushindwa kupeleka watoto wao shule kwa wakati kwa sababu wazazi
wengi wana kipato cha chini.
Michango
iliyoondolewa ni pamoja na michango ya Majengo, masweta na sare za shule.
Mkuu wa Mkoa
alikieleza kikao kuwa, pamoja na maamuzi hayo, serikali itapeleka maelekezo
katika bodi na kamati za shule ziwasilishe Mkoani aina yoyote ya michango
iliyokubalika katika vikao vya bodi na kamati hizo ili Mkoa uidhinishe michango
hiyo kama ina umuhimu.
Aidha,katika
kikao hicho serikali ya mkoa wa Shinyanga imeazimia kuboresha Elimu katika mkoa
huu kwa kuanza kufanyia kazi baadhi ya changamoto na kisha kufanya tathmini
baada ya mwaka mmoja kwa lengo la kumaliza tatizo moja baada ya lingine.
Changamoto
zilizopewa kipaumbele ni Kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni, kuongeza
idadi ya walimu hasa maeneo ya vijijini na kuimarisha idara ya ukaguzi wa shule,
pia, kukamilisha idadi ya madawati ya kutosha, kuthibiti utoro na mimba kwa
kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaosababisha utoro kwa wanafunzi na
wanaowapa mimba pamoja na kuongeza motisha kwa walimu waajiriwa wapya
wanaoripoti.
Mkuu wa Mkoa
pia amewazawadia wanafunzi waliofanya vizuri katika ngazi ya mkoa katika
mitihani ya Mwaka jana 2012 darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita
pamoja walimu wao waliofanyan vizuri.
Akifunga
kikao hicho amewataka wadau wote kusimamia sheria zilizopo kwa kila mmoja
kuwajibika katika sehemu yake, hususani Maafisa Elimu wa Wilaya amewataka
wasifanye kazi kwa mazoea.
No comments:
Post a Comment