HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 13, 2013

Miaka 35 ya Mashujaa, JWTZ bado ni la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania?

Na Bryceson Mathias
 
 
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linaadhimisha siku ya mashujaa kila tarehe 25 Julai, ikiwa ni sehemu ya kuwakumbuka Mashujaa waliopigana na kushinda vita ya Kagera mwaka 1978/1979.
 
Maadhimisho hayo yanayofanyika mara moja kwa mwaka,  taarifa ya Kurugenzi ya Jeshi hilo kwa Vyombo vya habari imesema, mwaka huu yatafanyika  Julai 25, 2013 katika Mkoa wa Kagera Wilaya ya Bukoba kwenye makaburi ya Mashujaa yaliyopo Kaboya.
 
Imeelezwa, Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, ambapo Sambamba na mgeni rasmi, watakuwepo viongozi waandamizi wa Serikali, vyombo vya Ulinzi na Usalama, vyama vya siasa, taasisi za Dini na taasisi mbalimbali za kiraia.
 
“Vyombo vya habari vinaalikwa kushiriki katika maadhimisho hayo ambayo ni muhimu kwa Taifa”.ilisema  taarifa hiyo Iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi, Upanga SLP 9203, Simu: 0764742161, Email:ulinzimagazine@yahoo.co.uk ya Julai 1. 2013.
 
Nikiwa mmojawapo wa washiriki wa vita ya Kagera mwaka 1978/1979 hadi kufika maili kadhaa ndani ya Sudan kuyafukuza Majeshi ya Fashisti Idd Amin, nafarijika sana kuona wapiganaji hao wanaenziwa, kutokana na upendoo wa upeo waliuoonesha kwa Watanzania.
 
Lakini, napata tabu na kujihoji! Je, Miaka 35 ya Mashujaa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania bado ni lile la Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere lililojikita kwa upendo na Ulinzi wa Mipaka ya Wananchi wa Tanzania au kuna Mapungufu kimaadili?
 
Nakumbuka JWTZ ya wakati wa Mwalimu, tulikuwa tukisikia Mwananchi Kapigwa au kuonewa na Mtu au Kataifa Jirani, basi tulikuwa tunalia kwa kuonewa kwake, na kilichofuatia ilikuwa ni Songombingo kumtetea Raia na Mwananchi, maana walikuwa kitu muhimu.
 
Kwa nini raia walikuwa muhimu! Wananchi walilipenda na kuliamini sana JWTZ na mwananchi ilikuwa rahisi kutoa siri yoyote kwa Askari wa JWTZ kuliko hata Polisi kutokana na uhusiano mzuri uliokuwepo, ambapo hata adui akiingia mpakani, ghafla alifahamika kaingia nchini.
 
Je, tunapoadhimisha miaka 35 ya kukumbuka Mashujaa wetu waliokataa udhariri wa Amin, uaminifu ule wa JWTZ bado upo hata leo? Au umepotezwa mbali na kupakazwa Mafuta ya Bunduki ya Siasa?
 
Mwanajeshi wa Miaka hiyo, alimuheshimu raia kama msaada wake wa Vita kama Askari anavyoiheshimu Silaha na Kibuyu chake cha Maji kiunoni au Askari wa Kikosi cha Mbwa anavyoheshimu Mbwa wake anayemuongoza kwa Adui, au Askari wa Farasi anavyoheshimu Farasi!
 
Ilikuwa ni mwiko kumsikia Askari wa JWTZ amempiga Raia au kumshambulia harafu akaachwa atambe barabarani au kambini! Askari huyo alihukumiwa Hukumu ya Kijeshi (Court Martial) na kufukuzwa Jeshi kwa aibu. Je leo hii hayo yapo?
 
Tumekuwa tukisikia mikoa mbalimbali ya nchi, Askari wa JWTZ wanawapiga raia (wananchi) kiasi cha hata kuwatesa, kudhulumu mali zao. Je nani atawaambia Adui wakiingia mipakani na kujificha kwa kujichanganya nao kama mnawafanyia hivyo?
 
Ni rai yangu, Maadhimisho ya mika 35, tukiona Makabauri ya ndugu zetu waliokufa kwa ajili ya kuwakomboa watanzania na aibu ya Amin, tukumbuke kurejesha Uhusiano mwema na Amani baina ya JWTZ na Raia kama enzi ya Mwalimu Nyerere, badala ya kudanganywa na watawala na kutumika vibaya kisiasa, kushambulia,kuwajeruhi na kuwaua raia na kumwaga damu zao!
 
 Nitafurahi kama mtakuwa kama Jeshi fulani la Afrika (Silitaji) ambalo lilikataa kuwashambulia na kuwatawanya wananchi na kuweka Silaha zao chini, wakitambua kufanya hivyo ni kuwakaidi na kuwafanyia wazazi na Ndugu zao wa Damu!
 
nyeregete@yahoo.co.uk0715933308

No comments:

Post a Comment

Pages