HABARI MSETO (HEADER)


September 29, 2013

MKAZI WA KISARAWE ADAIWA KUMG'ATA MWANAYE

Na Mwandishi Wetu, Kisarawe

WAKAZI wa Mlongazila wilayani Kisarawe mkoani Pwani wamelitaka jeshi la polisi kumkamata Moshi Hamad, kwa madai ya kumng’ata mwanaye wa kumzaa Khadija Twaha (6), sehemu za siri, akidai amekuwa akijisaidia haja kubwa na ndogo hovyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wilayani hapa juzi, wakazi hao, walisema mama huyo amekuwa na tabia ya kumfungia ndani mtoto wake huku akimchapa zaidi ya nusu saa jambo lililosababisha watoe taarifa kwenye dawati la haki za binadamu.

Walisema walifikia uamuzi huo baada ya kuchoshwa na vitendo hivyo ikiwemo kumpiga mwanaye huyo kwa kutumia nyaya za simu huku akimng’ata sehemu mbalimbali za mwili wa mtoto huyo na kumsababishia maumivu makali.

 Stella Musa alisema sehemu za siri za mtoto huyo zimeharibiwa kutokana na kung’atwa na meno huku sehemu zake za  makalio zikiwa na vidonda ambavyo vinadaiwa  vimetokana na kuchomwa na  ncha kali.

“Wazazi wa mtoto huyu ni wanangu, siku moja mama wa huyu mtoto alishawahi kumuumiza mkono nilimchukua na kukaa naye nyumbani kwangu kwa mwezi mmoja nikimuhudumia kwa kumkanda kwa maji ya moto,”alisema Stela.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Mlongazila ambaye ni katibu wa dawati la kutetea haki za binadamu Paulo Idana alisema suala hilo limewafikia hivyo wanachukua hatua za kisheria huku mtoto huyo akiwa chini yao kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Tulimfuata mama huyu Septemba 20 mwaka huu na kutulifanya mahojiano mbele ya ofisa Mtendaji wa kijiji hiki na alikiri akisema alifanya hivyo kwa sababu ya  hasira lakini, sisi msimamo wetu tunafanya utaratibu ili tuweze kumfikisha kwenye vyombo vya sheria,”alisema Idana.

Mtoto huyo, jina linahifadhiwa ambaye anasoma katika shule ya wali Mtenga (chekechea), alisema wakati mwingine mama yake alikuwa akimwiita ili amfundishe kusoma na aliposhindwa aling’atwa mgongoni, mapajani na sehemu za siri huku akisema atafanyia hivyo hadi ajue kusoma ndipo ataacha kumwadhibu.

 “Hivi vidonda vya kwenye mwili wangu ni vya kung’atwa wakati mwingine napigwa na waya, hiki kidole mama alinikata kutokana tu nilishindwa kusoma, alisema huku akilia kwa maumivu makali sana mtoto huyo.

Mama wa mtoto huyo, Moshi Hamad, alisema alikuwa akitoa adhabu hiyo  kwa mwanaye huyo  kutokana  kujisaidia haja ndogo na kubwa  hovyo wakati arudiopo kutoka shule.

“Nafanya hivi kutokana na hasira siwezi nikamuona mtoto wangu anajisaidia haja kubwa na ndogo kwenye nguo nikamwacha tu lazima nimwadhibu mbona, kama jana alitapika kwenye sahani je mtoto kama huyu nitamwacha,”alihoji Moshi.


Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Hadija Samizi alikiri kuwepo suala hilo hivyo serikali ya mtaa huo inafanya utaratibu ili kuhakikisha anafikishwa kwenye vyombo sheria.

No comments:

Post a Comment

Pages