REDD’S Miss Tanzania
2012/2013, Brigitte Alfred ambaye pia alifanikiwa kushika nafasi ya tatu katika
shindano la Beauty With a Purpose wakati wa kuwania taji la dunia (Miss World)
mwaka huu, amerejea nchini na kuwashukuru Watanzania kwa kumuunga mkono kwa
kipindi chote alichokuwa akishikilia taji hilo.
Brigitte alifanikiwa
kushika nafasi hiyo katika shindano hilo, ambalo lilishirikisha warembo zaidi
ya 190 kutoka sehemu mbalimbali duniani, ambalo lilikuwa mahususi kwa warembo
kuonyesha kazi walizofanya kwa jamii katika nchi wanayotoka.
Mrembo huyo alionyesha
jinsi alivyosaidia kwa kiasi kikubwa kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji
maalumu hasa wale wenye ulemavu wa ngozi.
Akizungumzia kuhusu
shindano la Miss World alisema, lilikuwa na changamoto nyingi na anaamini ni
lazima Watanzania wajivunie mafanikio ambayo yamefikiwa mpaka sasa katika
mashindano hayo ya dunia.
Mafanikio makubwa zaidi
ambayo Tanzania iliwahi kuyapata ni pale Nancy Sumari alipofanikiwa kutwaa taji
la Miss World Africa katika mashindano yaliyofanyika mwaka 2005.
Kuhusu kipindi chote
alichokuwa akishikilia taji la Redds Miss Tanzania alisema, alipata ushirikiano
mkubwa na akatoa shukrani kwa jamii kumuunga mkono kwa kipindi chote hicho.
“Napenda kutoa shukrani za
dhati kwa Kamati ya Redd’s Miss Tanzania, wazazi wangu, vyombo vya habari,
Serikali na Watanzania kwa ujumla kwa kuniunga mkono kwa kipindi chote hicho.
“Kusema kweli sina cha
kuwalipa na naahidi nitaendelea kushirikiana na kamati hii katika kuhakikisha
Tanzania inafanya vyema zaidi katika mashindano ya dunia siku za baadaye,”
alisema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya
Lino International, Hashim Lundenga ambao ndio waandaaji wa Redd’s Miss
Tanzania alisema, wanajivunia kwa kiasi kikubwa mafanikio yaliyofikiwa na
Brigitte katika mashindano hayo.
“Kwetu tunachukua fursa
hii kuyaomba makampuni au taasisi mbalimbali kujitokeza kudhamini mashindano
haya kwani ni muhimu zaidi kwa ustawi wa Taifa,” alisema.
Taji la Redd’s Miss
Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Happiness Watimanywa ambaye alifanikiwa
kulitwaa hivi karibuni.
Shindano la Redd’s Miss
Tanzania linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na
kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).


No comments:
Post a Comment