Watoto yatima wa kituo cha Tosamaganga jimbo la Kalenga wilaya ya Iringa wakimpongeza Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ujenzi wa barabara mkoani Iringa ya GNSM Contractrors Co. Ltd Bw Geofrey Mungai kulia kwa kuwajali kwa msaada wa chakula chenye thamani ya zaidi ya Tsh milioni 1.5 kwa ajili ya mwaka mpya. (Picha na Francis Godwin)
Na Francis Godwin,Iringa
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ujenzi wa barabara mkoani Iringa ya GNSM Contractrors Co. Ltd Bw Geofrey Mungai amekabidhi msaada wa chakula cha mwaka mpya chenye thamani ya zaidi ya Tsh milioni 1.5 kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Tosamaganga katika jimbo la kalenga wilaya ya Iringa vijijini .
Akikabidhi msaada huo leo Mungai alisema kuwa amelazimika kufika katika kituo hicho ambacho kinasimamiwa na masisita wa kanisa la RC kama sehemu ya mwendelezo wa kampuni yake kuendelea kuzungukia vituo mbali mbali vya kulea yatima na kuwapa faraja hasa katika msimu huu wa sikikuu.
Alisema kuwa miongoni mwa vituo ambavyo amepata kuvikumbuka katika msimu huu wa sikukuu ya Krismas na Mwaka mpya ni pamoja na kituo cha Daily Bread Life (DBL) kilichopo jimbo la Iringa mjini na kituo hicho cha Tosamaganga kilichopo jimbo la Kalenga huku lengo likiwa ni kuwakumbuka yatima hao na kuihamasisha jamii kuelekeza nguvu zao kwa yatima kama hao.
Bw Mungai alisema kuwa takwimu za maambukizi ya VVU katika mkoa wa Iringa zimeendelea kuongezeka na iwapo jamii haitajenga utamaduni wa kujali yatima vifo vya watoto yatima ambao watakosa chakula baada ya kupoteza wazazi wao kwa VVU pia vitazidi kuongezeka hivyo lazima misingi ya kuwajali yatima ikaanzwa kuwekwa mapema zaidi.
" Hawa watoto iwapo jitihada za vituo vya kusaidia yatima visinge kuwa na moyo huo leo yawezekana baadhi yao wasingekuwepo hapo tungekuwa tumewazika ila kazi nzuri ya kujitolea inayofanywa na vituo vya yatima ndio imewafikisha hapa leo ....hivyo lazima sisi kama jamii kuunganisha nguvu zetu na vituo vya yatima"
Pia alisema kuwa hata viongozi wa vyama vya siasa na serikali ni vema wakaweka utaratibu wa kufanya ziara za mara kwa mara katika vituo vya yatima na kujifunza mazingira ambayo watoto hao wanaishi ikiwa ni pamoja na kusaidia kutatua changamoto zinazovikabili vituo vya yatima mkoani Iringa .
Kwani alisema kwa upande wake kama mkandarasi ambae amekuwa akifanya kazi ya ujenzi wa barabara mkoani Iringa na nje ya mkoa ameona ni vema katika fedha kiasi ambazo anazipata kuweka utaratibu wa kusaidia watoto yatima kama njia ya kuwahamasisha pia wenzake kujitoa kwa yatima katika maeneo yao ama kusaidia kuchangia maendeleo ya maeneo yao.
Katika hatua nyingine Mungai aliwapongeza walezi wa vituo vya yatima katika mkoa wa Iringa kuwa kutokana na mchango wao wa kulea yatima hata idadi ya yatima na watoto wa mitaani katika mji wa Iringa imeonekana kupungua zaidi
Kwa upande wake diwani wa viti maalum tarafa ya Kalenga Shakra Kiwanga akimpongeza Mungai alisema kuwa ameonyesha upendo mkubwa kwa yatima hao na kuwataka makandarasi wengine kuiga mfano huo.
Kiwanga ambae pia ni mmoja kati ya makandarasi wadogo mkoani Iringa alisema kuwa alichofanya Mungai ni somo kwao pia katika kutoa sehemu ya makusanyo wanayoyapata kupitia kazi mbali mbali.
Awali mlezi wa kituo hicho Herena Kihwele alisema kuwa kituo hicho kina watoto zaidi ya 100 na kuwa kwa sasa kituo kinakabiliwa na changamoto kubwa ya kushindwa kuwalipia ada sekondari watoto zaidi ya 10 waliofaulu darasa la saba ila kituo hakina uwezo wa kuwasomesha .
Iwapo umeguswa kuchangia kituo hicho ada ama msaada wowote ule waweza kuwasiliana na mlezi wa kituo hicho Sisita Herena Kihwele kwa simu 0768831477 pia waweza kutumia namba hiyo kwa kutuma M-PESA.
No comments:
Post a Comment