KIPIGO cha mabao 3-1 ilichopata Yanga katika mechi ya Nani Mtani
Jembe katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Desemba 21, kimegharimu kibaru
cha aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mdachi, Ernie Brandts (pichani).
Brandts, beki wa zamani wa PSV Eindhoven ya Uholanzi aliyetua Yanga
mwanzoni mwa msimu uliopita akiziba nafasi ya Tom Saintfiet, ameondoka akiwaachia
ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, pia wakiongoza raundi ya kwanza ya ligi hiyo
ikifuatiwa na Azam, Mbeya City na Simba.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Mashindano ya klabu ya Yanga, Abdallah Binkleb alisema, wamefikia uamuzi huo kutokana na timu
kushuka kiwango kila kukicha, licha ya kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa.
Alisema uongozi ulishampa ‘notice’ ya siku 30 kuelekea kusitisha
mkataba wake ili waweze kusaka kocha mwingine ambaye atakuwa na uwezo zaidi
kwani kiwango cha timu yao dimbani kinasikitisha kwa sasa.
“Tumeishamwandikia barua tangu leo ya kuachana naye, hivyo
basi tunaanza mchakato wa kutafuta kocha mwingine, tutaendelea kuwapa taarifa
zaidi juu ya bechi hilo la ufundi,” alisema Binkleb na kuongeza kuwa kiwango
kilichooneshwa na timu yao ni cha kusikitisha.
Alisema, maamuzi hayo yanatokana na mwenendo usioridhisha wa timu
hiyo katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu, kirafiki na bonanza la Nani Mtani
Jembe dhidi ya Simba SC mwishoni mwa wiki huku akiwapongeza, Simba kwa kuibuka
na ushindi mnono katika mchezo huo.
“Uamuzi huu dhidi ya Brandts, usichukuliwe kama chuki, bali ni moja
ya sehemu ya kuboresha benchi la ufundi ili tuweze kupata matokeo mazuri uwanjani
katika mashindano ya kitaifa na kimataifa yaliyo mbele yetu,” alisema.
Mbali ya kukabiliwa na vita ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu, pia Yanga
itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikianzia hatua ya awali dhidi ya
Komorozine ya Comoro na mshindi wa hatua hiyo, atakutana na mabingwa watetezi
wa michuano hiyo, Ahly ya Misri.
“Ukitazama uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa Yanga na wapinzani wetu,
pia soka tuliyocheza Jumamosi, kwa kweli ni dhahiri mwalimu amefikia mwisho
kimbinu, hana njia mbadala,” alisema.
Aliongeza kuwa hata kabla ya mechi ya Jumamosi, Yanga imekuwa
ikicheza chini ya kiwango katika michezo ya Ligi Kuu ndio maana imekuwa ikipata
ushindi kwa mbinde na pengine kufungwa, hivyo wamechukua uamuzi huo mgumu kwa
maslahi ya timu.
Alisema chini ya ‘notisi’ ya siku 30, Brandts ataamua mwenyewe kama
ataendelea kusimamia mazoezi
ya timu hiyo ndani ya kipindi hicho ama kuondoka moja kwa moja kabla
ya muda kufikia ukomo.
Katika mechi hiyo ya Nani Mtani Jembe iliyochezeshwa na Ramadhan
Ibada wa Zanzibar, mabao ya Simba yalifungwa na Amis Tambwe aliyecheka na nyavu
mara mbili na jingine likiwekwa wavuni na Awadh Juma huku Ramadhan Singano
‘Messi’ akitoa mchango mkubwa katika mabao hayo.
No comments:
Post a Comment