HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 24, 2014

SERIKALI YAWATAKA WADADISI WA UTAFITI KUZINGATIA WELEDI

Na Mwandishi Wetu 

SERIKALI imewataka wasimamizi na wadadisi wa Utafiti wa Tathmini ya Utoaji wa huduma za Afya nchini mwaka 2014/15 kuzingatia weledi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuepuka  kukusanya takwimu zisizo wakati wa utafiti huo utakaofanyika nchi nzima kuanzia Oktoba 13 mwaka huu. 

Aidha,, imewaagiza Waganga Wakuu wa MikoaWilayamadakatari na wafanyakazi wa vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini  kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaoendesha utafiti huo ili waweze kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika maeneo yao kwa lengo la kupata taarifa sahihi  zitakazofanikisha utafiti huo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku 27 kwa wakufunzi na wadadisi  kutoka  Tanzania Bara na Zanzibar watakaoendesha  utafiti huo mjini Moshi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif Rashid alisema kuwa wakufunzi, wadadisi na wataalam  hao wanayo nafasi kubwa ya kufanikisha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazotoa taswira halisi ya utoaji wa huduma ya afya nchini kwa mwaka 2014/2015.

Alisema utafiti huo utaiwezesha serikali kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali nakufikia malengo iliyojiwekea kitaifa na kimataifa kwa kuboresha na kuendelea  kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wake.

Dk ashid, alisema Serikali imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali za kuboresha huduma za afya na maisha ya Watanzania kwa kupitia Mikakati ya Kimataifa na Kitaifa ikiwemo ile ya Malengo ya Milenia ya Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011 -2016).

Aliizitaja programu nyingine kuwa ni pamoja ile ya Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA) na Mkakati wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA) kwa upande wa Zanzibar. 

Dk. Seif, alisema katika juhudi hizo, Wizara ya hiyo imekuwa na jukumu la kusimamia programu mbalimbali za afya na kufuatilia utekelezaji na utoaji wa huduma za afya nchini.

Alieleza kuwa wakati wa utafiti wa kwanza wa Kutathmini Utoaji wa Huduma za Afya nchini unafanyika na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2006,Tanzania ilikuwa na  jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 5669, kati ya hivyo 224  zilikuwa ni hospitali, 541 vikiwa ni vituo vya afya na zahanati 4904. 

Amesema kumekuwa na maboresho makubwa katika sekta ya afya hadi kufikia mwaka 2013 ambapo takwimu zinaonyesha kuwepo kwa  vituo  6767 vya kutolea huduma ya afyanchini , hospitali 256, vituo vya afya 701 na zahanati 5810.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa akizungumzia mafunzo hayo amesema kuwa washiriki watakaofaulu na kukidhi vigezo vilivyowekwa  watashiriki katika zoezi la kukusanya takwimu za utafiti huo  kwa kipindi cha miezi minne kuanzia  tarehe 13 Oktoba 2014 .

Alisema utekelezaji wa utafiti huo na mafunzo hayo unafanywa kwa pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii - Tanzania Bara, Wizara Afya - Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Shirika la ICF International la Marekani ambao pia wanatoa ushauri wa kitaalamu katika kufanikisha utafiti huo.

No comments:

Post a Comment

Pages