HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 25, 2014

TAIFA STARS, BENIN KUCHEZA DAR OKTOBA 12

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inashuka uwanjani Oktoba 12 mwaka huu kuikabili Benin katika mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Programu ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya mechi hiyo itatangazwa baadaye na Kocha Mkuu Mart Nooij.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea na taratibu nyingine kwa ajili ya mechi hiyo ikiwemo usafiri wa Benin kuja nchini, ambapo timu hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Oktoba 10 mwaka huu ikiwa na msafara wa watu 28.

Pambano la Stars na Benin litatanguliwa na mechi ya kudumisha upendo kati ya viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu.

Wakati huo huo, kutokana na mechi hiyo ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inafanyiwa marekebisho madogo, na marekebisho hayo yatatangazwa kesho (Septemba 26 mwaka huu).

RAIS MALINZI KUFUNGA KOZI YA WANAWAKE
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi anatarajia kufunga mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa vyama vya mpira wa miguu wa wanawake vya mikoa ya Tanzania Bara.

Hafla ya kufunga mafunzo hayo itafanyika kesho (Septemba 26 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Mafunzo hayo ya siku tano yalishirikisha viongozi 34 wakiwemo baadhi ya waandishi wa habari na Meneja wa Twiga Stars, na yaliendeshwa na Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Henry Tandau.

BONIFACE WAMBURA
KNY KATIBU MKUU
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Pages