HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 23, 2014

TANESCO NA MIRADI NA UMEME

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Mhandisi, Felchesmi Mramba, amesema baada ya kukamilika miradi mingi iliyoanzishwa ya ufuaji umeme katika kila mkoa, tatizo la umeme linatarajiwa kutoweka kabisa nchini.

Akizungumza na wandishi wa habari wakati ziara kutembelea baadhi ya miradi ya ujenzi wa vituo saidizi vitano vya usambazaji umeme jijini Dar es Salaam, Mramba, alisema vituo hivyo vitasaidia kulifanya jiji hilo kuwa na umeme wa uhakika.

Baadhi ya vituo hivyo walivyotembelea wandishi hao wa habari ni Mbagala, Gongolamboto na Kinyerezi.

Alisema kuwa matarajio hayo yanatokana  na miradi hiyo ambapo, Tanesco imejiwekea malengo kwamba hadi ifikapo mwisho mwa mwaka 2015 iwe imezalisha megawati 3000, ambazo ni umeme wa uhakika.

Mramba, alisema ukichukuwa kuanzishwa kwa miradi hiyo mingi ambayo iko karibu nchi nzima, utaona umeme utakaozalishwa ni zaidi ya megawati 3000 ambazo zitakuwa ni nyingi.

“Kusema kuwa Tanesco itaweza kuitekeleza miradi hiyo pekee hiyo si kweli kutokana na kuhitajika fedha nyingi bali itakuwa ikishirikiana na sekta binafsi ambazo zipo ambazo zimejitokeza mfano ni NSSF na nyingine za kutoka nje,”alisema Mhandisi Mramba.

Aliitaaja baadhi ya miradi hiyo mikubwa kuwa ni ile ya kuzalisha na kusafirisha umeme ambapo vyanzo vyake vikubwa ni gesi, makaa ya mawe na maji.

Mramba, alisema kwa sasa nguvu kubwa imeelekezwa katika umeme wa gesi, mfano ni mradi mkubwa uliyoko katika eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam, ambako kuna miradi minne ambayo imepewa majina ya Kinyerezi namba moja hadi nne.

“Nyinyi ni mashihidi kuwa miaka mitatu, minne iliyopita kulikuwa na mgao amabo ulikuwa unakwenda hadi saa 12 na kila mtu jijini alikuwa wakitumia jenereta na Inveta lakini nadhani mtakubaliana na nami kutokana na mafanikio yaliyofanywa na Tanesco tatizo la kukatika umeme jijini kama awali haliko tena,”alisema Mramba.

Meneja Miradi, Ufuaji Umeme, Mhandisi, Simon Jirima, alitaja uwezo wa uzalishaji wa kila miradi akisema Kinyerezi namba moja utakuwa na uwezo wa megawati 150 namba mbili megawati 240, namba tatu megawati 600 na namba nne megawati 332.

Alisema ujenzi wa Kinyerezi namba moja umefikia asilimia 90 ya manunuzi ya vifaa na katika ujenzi uko katika asilimia 70, na kwamba unatarajiwa kukamilika Januari mwaka ujao na makabidhiano rasmi itakuwa Machi mwaka huo huo.
Mhandisi Jirima, alisema kukamilika kwa miradi huo kutaondoa kero katika maeneo kama vile Kimara na kwingineko.

No comments:

Post a Comment

Pages