HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 11, 2014

WAHITIMU WA DARASA LA SABA IRINGA WAJIHAKIKISHIA UFAULU MZURI MTIHANI WA TAIFA, WAWATAKA WAZAZI WAJIPANGE KUWAPELEKA SEKONDARI

Mhitimu wa darasa la saba   shule ya Msingi Muungano  mjini  Iringa  aliyejitambulisha kwa jina moja la Emanuel akifuatilia tangazo la masomo ya  ziada (TUITION) kwa ajili ya  kidato  cha kwanza tangazo lililobandikwa katika   nguzo ya simu  eneo la Danish mjini Iringa  baada ya kumaliza kufanya mtihani wa Taifa wa darasa la  saba.
Mwanafunzi  Andason Aldoph ,Salma Yusuph na Naufary Rajab wakishangilia  baada ya  kuhitimu  elimu ya msingi  leo
Wahitimu wa darasa la saba katika  shule ya msingi  Lugalo na Wilolesi mjini  Iringa  wakijipongeza kwa kushangilia baada ya  kumaliza kufanya mtihani wa Taifa wa darasa la  saba  jana huku  wakiimba  wimbo  wao kuwa wamemaliza viboko  sasa  basi ufaulu ni lazima kama  walivyokutwa na mpiga picha  wetu  leo jioni
 
Na Francis Godwin Blog 

BAADHI ya  wahitimu wa  darasa la  saba  waliomaliza  kufanya mtihani  wa Taifa  leo  mjini  Iringa  wamejihakikishia   ushindi mkubwa katika mtihani wa mwaka huu .

Wakizungumza na mtandao huu wa www.matukiodaima.co.tz leo  mara baada ya  mtihani  huo  wanafunzi hao kutoka  shule ya msingi Muungano , Lugalo na Wilolesi  walisema  kuwa mitihani  hiyo  walioyoifanya  ni ya kawaida  sana na  hivyo uwezekano mkubwa wa  kufaulu  upo .

Mwanafunzi  Andason Aldoph ,Salma Yusuph na Naufary Rajab  waliozungumza na mwandishi wa habari hizi  walisema  kuwa awali  walikuwa na  hofu  kubwa  kama  mtihani  huo  ungekuwa mgumu  zaidi ila  baada ya  kuanza mitihani  hiyo juzi  hadi jana  walipomaliza  hakuna swali  jipya  zaidi ya yale  waliyofundishwa katika masomo  yao.

" Tunaomba   wazazi  waanze  kujiandaa kwa ajili ya kutupeleka  sekondari  kwani tunao uhakika mkubwa  wa kufaulu katika mtihani  huu tena kwa asilimia 100 zote"  walisema  wanafunzi   hao  kutoka shule ya Msingi Lugalo 

Wakati  mwanafunzi  Rahab   kutoka  shule ya  Msingi  Wilolesi  alisema  kuwa  kwa upande  wake  amekuwa mbele ya  wenzake kwa  zaidi ya  dakika  20 kumaliza mtihani  huo na  hivyo mategemeo yake  kufanya  vizuri  zaidi na  sekondari kwake ni lazima.

Huku  mwanafunzi  Mlinge  Abass kutoka  shule  ya Msingi Lugalo  akidai kuwa  mavuno ya  miaka  7  waliyokuwepo  shuleni  wanategemea  kuyavuna  baada ya  matokeo ya mtihani huo ambao hata  hivyo kwake ana matumaini makubwa wa  kufaulu .

Kwa  upande wake  mwanafunzi  wa shule ya msingi Muungano aliyejitambulisha kwa  jina moja la  Emanuel alisema kuwa  kutokana na mtihani  huo kuwa wa kawaida  zaidi  upo uwezekano wa wanafunzi  wengi  zaidi  kufanya  vema mwaka  huu tofauti na  matokeo ya mwaka jana.

Hata  hivyo  uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa tayari  ulikwisha anza maandalizi ya vyumba vya madarasa katika shule mbali mbali za  sekondari mjini hapa  ili  kuwezesha  wanafunzi  watakaofaulu  kuweza  kujiunga na  kidato  cha kwanza kwa wakati.

Akizungumza katika  kikao cha baraza la madiwani  kilichofanyika hivi karibuni  pamoja na mambo mengine mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa Aman Mwamwindi  aliwataka  madiwani  kuendelea  kusimamia ujenzi wa  vyumba  vya madarasa katika  shule  zote za  sekondari na kuwa lengo la Manispaa ni kuona  wanafunzi wote wanajiunga na sekondari hasa ukizingatia kuwa Manispaa  hiyo  ndio ambayo  imekuwa ikishika nafasi ya  kwanza kwa  ufaulu  kila mwaka.

No comments:

Post a Comment

Pages