Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri (aliyesimama) akimkaribisha mgeni rasmi Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bibi Mwantumu Mahiza (aliyekaa kaikati). Kulia ni Katibu wa Baraza hilo Bw. Senya Robert. Picha na: Thomas Nyindo, Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.
Wajumbe wa baraza wakiwa katika
hali ya utulivu katika kufuatilia na kuchangia mada mbalimbali wakati wa kikao
hicho. Walioketi meza ya mbele kutoka kulia ni Bw. Paul Sangawe, Bw. Dunstan
Nyeme, Bw. Abdul Nungu na Bi. Catherine Mbilia.
Wengine walioketi meza ya nyuma kutoka kulia ni Bw. Saulo Fisoo na Bw. Paul
Masibuka.
Wajumbe wa Baraza wakifuatilia kwa makini majadiliano yaliyokua yakiendelea wakati wa baraza hilo.
Mgeni Rasmi wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mwantumu Mahiza (aliyesimama) akisisitiza jambo alipokua akifungua kikao cha Baraza hilo.
Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi Ofisi ya Rais, Tume ya Mipando kwa pamoja wakiimba wimbo wa Solidarity Forever kuonyesha mshikamano makazini.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi, Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakionyesha mshikamano kwa kuimba wimbo wa Solidarity forever mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kufungua rasmi kikao hicho.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi, Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi. Mwantumu Mahiza (Walioketi wa pili kushoto). Walioketi pamoja nae kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Bibi Florence Mwanri, Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Mipango, Bw. Steven Katemba na Katibu wa Baraza Bw. Senya Robert.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA PWANI MH. MWANTUMU
BAKARI MAHIZA KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA OFISI YA
RAIS, TUME YA MIPANGO KATIKA UKUMBI WA HOTELI YA JD COMPLEX – KIBAHA, PWANI.
Awali ya yote napenda
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwepo hapa leo hii tukiwa na afya
njema. Pia, nikushukuru wewe binafsi Kaimu
Katibu Mtendaji, pamoja na timu yako kwa kunipa heshima hii kubwa ya kuwa mgeni
rasmi katika ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango.
Ndugu
washiriki,
Nimearifiwa kuwa Baraza
hili ni la kwanza katika mwaka 2014/15 na limewakilishwa na Wakuu wote wa
Klasta, Idara na Vitengo, wajumbe wa TUGHE Taifa, TUGHE Mkoa – Dar es salaam,
Halmashauri ya Tawi la TUGHE Tume ya Mipango na mjumbe mmoja mmoja kutoka kila
Klasta, Idara na Vitengo.
Aidha, napenda kutumia
fursa hii kuwapongeza wajumbe wote wa mkutano huu kwa kuchaguliwa kwenu kuwa
wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kupitia
mabadiliko ya Mkataba Mpya. Hii ni kutokana na imani kubwa waliyonayo watumishi
juu yenu katika kuwawakilisha katika chombo hiki muhimu.
Ndugu
washiriki,
Baraza la Wafanyakazi ni
kama Bunge la Taasisi yenu kwa kuwa linaundwa na wawakilishi wa wafanyakazi
wote waliochaguliwa kidemokrasia. Baraza
hili ni chombo muhimu sana kilichoundwa kisheria kwa madhumuni ya kuwashirikisha
watumishi katika kujadili na kufanya maamuzi kuhusu masuala yanayohusu maslahi
ya ajira mahali pa kazi kwa lengo la kuleta tija. Kupitia Baraza hili mwajiri
anapokea maoni ya watumishi na kuweza kufikia maamuzi sahihi ya namna ya
kuboresha mazingira ya kazi na watumishi kwa ujumla.
Wajibu wa mabaraza haya
kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi
wanatambua wajibu na haki zao na wanazingatia maadili ya utumishi wao ili
kuleta matokeo makubwa ya utendaji kazi yenye tija.
Ndugu
washiriki,
Hata kama kutakuwa na sera,
sheria na kanuni nzuri katika mahali pa kazi pasipokuwa na ushirikiano baina ya
mwajiri na watumishi itakuwa vigumu
Taasisi kutimiza malengo yake. Hivyo
pamoja na mambo mengine Baraza hili lina wajibu wa kuishauri Tume kwa lengo la
kuleta tija na mshikamano baina ya mtumishi na mwajiri. Sio vizuri kwa
watumishi kutumia muda mwingi katika kudai maslahi zaidi kuliko kupima kiwango
cha utekelezaji wa wajibu wao.
Moja ya kazi za Baraza ni
kuhakikisha kuwa watumishi wanatekeleza wajibu wao kwanza kabla ya kudai
maslahi na wanapodai maslahi wanatakiwa kufuata misingi ya sheria na taratibu
zilizopo.
Ndugu
washiriki,
Tume ya Mipango iliundwa
chini ya Ofisi ya Rais kutekeleza majukumu ya msingi ambayo ni kutoa dira ya
maendeleo na mwongozo wa uchumi wa taifa, kubuni na kuishauri Serikali kuhusu
sera za menejimenti ya uchumi na mikakati ya maendeleo na kufanya utafiti.
Ndugu
Mwenyekiti na washiriki;
Napenda kutumia nafasi hii
kukupongeza Mwenyekiti kwa kushirikiana na wasaidizi wako na watumishi wote kwa
ujumla kwa kuweza kutekeleza majukumu mliyopewa kitaifa kwa ufanisi. Nimeelezwa kuwa pamoja na changamoto za uhaba
wa rasilimali katika mwaka wa fedha 2013/14 mmeweza kutekeleza jukumu kubwa la
kutayarisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa, 2014/15 ambao uliwasilishwa katika
kikao cha Bunge cha mwezi Juni 2014, pamoja na majukumu mengine ambayo ni
kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14 na kufanya
mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 –
2015/16), kusambaza machapisho mbalimbali ya Tume ya Mipango na kuandaa
Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Management Manual).
Ndugu
Mwenyekiti na washiriki;
Ni matarajio yangu kuwa kwa
kuzingatia taratibu na miongozo ya Serikali, Tume ya Mipango mmepanga malengo
mbalimbali ya kutekeleza katika mwaka wa 2013/14 ambapo hatimaye mtakuwa kwenye
nafasi nzuri ya kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali ya kiuchumi,
kisiasa na kijamii. Kwa kusema hivi natumaini kuwa michango yenu katika mkutano
huu wa siku mbili, itatoa matokeo makubwa yatakayoliwezeshaTaifa letu kusonga
mbele kiuchumi.
Ndugu
Mwenyekiti na washiriki;
Hivyo, ni matumaini yangu
kuwa kwa kutumia kikao hiki kama wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi mnayo nafasi
kubwa ya kuwaelimisha wafanyakazi wenzenu kuhusu umuhimu wa kila mmoja kutimiza
wajibu wake katika sehemu yake ya kazi ili kufikia malengo mliojiwekea. Njia
pekee ya kufikia malengo yetu ni kila mmoja kufanya kazi kwa bidii na
kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kulitendea haki Taifa letu. Kila
mmoja wetu akemee kwa sauti watumishi wasiotimiza wajibu wao. Wakuu wa Klasta,
Idara na Vitengo wasimamie kwa dhati suala la maadili katika sehemu zao za
kazi. Tukumbuke kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huelekeza kuwa
kila mtu apate ujira unaolingana na wajibu aliotimiza.
Ndugu
Mwenyekiti na washiriki;
Nimeelezwa kwamba miongoni
mwa mada zitakazowasilishwa na kujadiliwa katika mkutano huu ni mafanikio ya
utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2013/14 na kujadili taarifa ya fedha za mwaka,
elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, umuhimu wa mawasiliano serikalini na
uelewa juu ya kiwango kinachopaswa kutozwa kodi ya mapato yatokanayo na ajira
(mshahara).
Ndugu
Mwenyekiti na washiriki;
Mwisho napenda kutoa
shukrani kwa kuwa Mgeni Rasmi katika mkutano huu muhimu na kuwatakia
majadiliano mazuri na yenye lengo la kuimarisha uhusiano mzuri kwenye Taasisi
yenu. Nihitimishe kwa kuwatakia kikao
chenye mafanikio yaliyokusudiwa.
Baada ya kusema hayo
machache, napenda kutamka kwamba ‘Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya
Mipango Umefunguliwa Rasmi’!
No comments:
Post a Comment