Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ,
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Mbwana . J. Mbwana akisalimiana na Rais wa
Umoja wa Vyuo vya Usafiri wa Anga Barani
Afrika(AATO) Tchagbele Sadamba wakati
wa mkutano mkuu wa kwanza wa AATO unaofanyika Zanzibar kwa ajili ya kujadili mbinu za
kuboresha mafunzo ya usafiri wa anga
barani Afrika. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Uchumi Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA)
Dkt. James Diu. (Na Mpiga Picha Wetu)
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa kwanza wa Umoja
wa Vyuo vya Mafunzo ya Usafiri wa Anga Barani Afrika (AATO)
utakaofanyika Zanzibar.
Mkutano huo wa siku tatu, kuanzia Oktoba 1-3, utakutanisha vyuo vya
mafunzo ya usafiri wa anga, wataalamu wa sekta na taasisi nyingine
zinazohusiana na masuala ya usafiri wa anga. Kauli mbiu ya Mkutano ni “Uhuishwaji na Viwango vya Mafunzo ya Usafiri wa Anga kwa Usalama wa Usafiri wa Anga Barani Afrika na Kwingineko”.
Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe atafungua mkutano huo
wakati, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano , Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Dkt Juma Duni Haji atakuwa mgeni rasmi wakati wa kufungwa kwa
mkutano.
Wakati wa mkutano huo wajumbe watajadiliana kuhusu ushirikiano wa
vyuo vya usafiri wa anga, hatua zilizofikiwa katika kuanzisha vituo vya
mfano(center of excellence) vya mafunzo ya usafiri wa anga na uhaba wa
wataalam wa usafiri wa anga barani Afrika, changamoto zinazotokana na
taaluma mpya za usafiri wa anga na mstakabali wa AATO.
Wajumbe hao pia watapata fursa ya kutembelea maeneo ya utalii huko
Zanzibar. Maeneo hayo ni pamoja na mashamba ya viungo, kisiwa cha Prison
maarufu kwa kobe wakubwa na eneo la mji mkongwe wa Zanzibar.
AATO ilizinduliwa mwaka 2013 huko Abuja, Nigeria kufuatia mapendekezo
ya mkutano maalumu wa Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO AFI-
RAN) mwaka 2008 nchini Afrika Kusini. Mapendekezo yalizitaka taasisi za
mafunzo ya usafiri wa anga kuwa na mikutano ya pamoja kwa lengo la
kuboresha ushirikiano, viwango, ubora na kuhuisha mafunzo ya usafiri wa
anga barani Afrika.
Malengo mkakati ya AATO ni pamoja na kuwa na sauti ya pamoja ya
vyuo wanachama na kuhimiza vyuo hivyo kuendeshwa kwa kuzingatia
viwango vya kitaifa na kimataifa.
Vyuo wanachama wa AATO vinapata manufaa mbali mbali ikiwa ni pamoja
na kuwa kwenye ushirikiano na vyuo wanachama, fursa ya kujitangaza na
kutambulika zaidi, kuwa na mitaala inayokidhi viwango. Faida nyingine ni
kupata taarifa sahihi kuhusu sekta ya usafiri wa anga
Chuo cha usafiri wa Anga Tanzania(CATC) ni miongoni mwa wanachama
waanzilishi wa AATO pia ni mwanachama wa baraza la AATO ikiwakilisha
nchi za Afrika Mashariki. AATO ina vyuo wanachama 30.
Margareth Kyarwenda
KNY
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA(TCAA).
No comments:
Post a Comment