Na Mwandishi Wetu
KUFUATIWA kukerwa na kitendo cha kupokwa kwa ushindi kwa mtu
waliyemchagua katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji
uliofanyika siku ya Jumapili, wakati wa Mtaa wa King'ongo uliopo Kata ya
Saranga, wilaya ya Kinondoni wamepanga kufanya maandamano sambamba na
kuifunga ofisi ya Uongozi wa mtaa huyo mpaka mtu waliyemchagulia
atakapopewa ushindi wake.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wakazi hao
wengi wakiwa na hasira, wamedai kuwa wamechukizwa na uhuni waliofanyiwa
na wasimamizi wa Uchaguzi wa Mtaa wao kwa kumtangaza kinyemela aliyekuwa
Mwenyekiti wa mtaa huo, Demetrius
Mapesi wakati mshindi halali waliyemchagua akiwa ni aliyekuwa Mgombea
wa UKAWA kupitia chama cha CUF, Aboubakar Nyamuguma.
Wananchi
hao walisema wapo katika kujiorodhesha majina kwa ajili ya kuandaa
maandamano kwenye ofisi za Manispaa ya Kinondoni kulalamikia waliouita
uhuni wa wasimamizi kutumia askari wa jeshi la Polisi kuwatawanya kwa
mabomu kisha kutangaza mshindi ambao aliangushwa kwa kura walizopiga.
"Walichelewesha
kutangaza majina baada ya kutokea sintofahamu, walipoona tumeamua
kuwakomalia wamtangaze mtu tuliyemchagua usiku wa saa 4 wakaita Polisi
wakaja kutupiga mabomu kisha wakamtangaza Mapesi kuwa kashinda bila
wagombea kusaini fomu wala kubandika mpaka sasa matokeo hayo ubaoni kama
inavyotakiwa, huu ni nini kama sio uhuni," alihoji mmoja wa wakazi hao
aliyejitambulisha kwa jina la Baba Ramadhani.
Alisema
pamoja na hila wanazofanya CCM za kutaka kulazimisha matokeo ili Mapesi
aendelee kuwa kiongozi wa eneo lao wameapa hawatakubali na ikiwezekana
wataifunga ofisi kwa makufuri mpaka Nyamuguma apewe ushindi wake kwa
sababu ndiye waliyemchagua.
Mgombea
anayedaiwa kuporwa ushindi, Aboubakar Nyamuguma alisema kuwa mpaka sasa
hajui kitu gani kilichotokea baada ya awali kukubaliana na msimamizi
kuziondoa kura zilizoonekana zimeongezeka kuliko idadi ya
waliojiandikisha na kupiga kura.
"Ilionekana
kura 32 zilizidi zaidi ya waliojiandikisha na kupiga kura ambao
walikuwa 930, baadaye tukakubaliana zilizozidi ziondolewe kama taratibu
zinavyotaka kisha zihesabiwe zinazopaswa na matokeo yalionyesha nimepata
kura 461 dhidi ya 431 za mpinzani wangu," alisema.
"Cha
ajabu baada ya kuona nimembwaga Mapesi Msimamizi na wasaidizi wake
ambao wengi ni walimu wanaofundisha Shule ya King'ongo ambayo mpinzani
wangu ni Mwenyekiti wa Kamati ya Shule waligoma kutangaza matokeo na
kusababisha wananchi kucharuka kabla ya kuita Polisi na kuwapiga watu
mabomu na kuwatawanya na kumtangaza Mapesi kuwa mshindi kwa kumpa kura
32 zilizoondolewa na hivyo kumfanya afikishe kura 463 dhidi ya zangu,"
alisema Nyamuguma.
Alisema
kitu cha ajabu msimamizi alitangaza matokeo bila hata wagombea kusaini
fomu kama inavyotakiwa na pia kutobandikwa ubaoni na kutokomea zake.
Aliongeza
kuwa kwa kutambua kuwa amepokwa haki yake ameandika barua ya pingamizi
dhidi ya kitendo hicho kwa Mratibu wa Uchaguzi Mkuu Kinondoni na nakala
kutuma katika ofisi zote zinazohusika ikiwamo kwa viongozi wake wa UKAWA
kuhakikisha haki inapatikana.
Alipoulizwa
kama ni kweli wapo watu wanaotaka kufanya maandamano alisema, hana
taarifa ila kama ni kweli ni uthibitisho kuwa wananchi hata wenyewe
wanasbabu ya kufanya hivyo kwani walimchagua ili awaongoze baada ya
kutoridhishwa na uongozi wa kiongozi aliyekuwapo awali.
No comments:
Post a Comment