Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Ubungo,
John Mnyika (Chadema), amezitaka Mamlaka ya Maji safi na Maji taka (Dawasa), na
Kampuni ya Maji safi na Maji taka (Dawasco), Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani,
kueleza ni lini mgawo wa maji utapungua jijini.
Mnyika alitoa
kauli hiyo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya mgawo wa maji
inavyoendelea katika jimbo hilo.
Mbunge huyo
alitoa kauli hiyo baada ya kugundua kuna mitaa ambayo mgawo wa maji haujarejea
katika hali ya kawaida, ndiyo maana akazitaka Dawasa na Dawasco watoe taarifa
kwa umma kwamba matatizo katika maeneo hayo yaliyobaki yatamalizika lini.
Aliyataja maeneo
ambayo yameathirika kuwa ni Jimbo la Ubungo na Segerea jijini Dar es Salaam na
Kibaha mkoani Pwani, yanayopata maji kutoka mtambo wa Ruvu Juu.
Mnyika alisema
kuna baadhi ya maeneo katika jimbo lake hali ya maji imeanza kurejea katika
hali ya kawaida, ambayo ni Kata ya Kibamba, Kwembe, Msigani, Mbezi Luis, Kimara,
Saranga, Ubungo na Makuburi.
Hata hivyo, alisema
katika kata hizo ipo mitaa ambayo mgawo haujarejea katika hali ya kawaida,
hivyo kuzitaka Dawasa na Dawasco zijitokeze kutoa taarifa kwa umma ni lini hasa
matatizo katika maeneo yaliyobaki yatamalizika.
“Aidha, namtaka
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, kujitokeza hadharani ili atoe taarifa
kwa umma kuhusu ripoti ya uchunguzi juu ya kujirudia rudia kwa matatizo ya maji
katika mtambo wa Ruvu Juu,” alisema.
Mnyika alisema
matatizo hayo yameathiri wananchi wa Ubungo na Segerea jijini Dar es Salaam na
Kibaha mkoani Pwani, hususan katika maeneo ambayo yanahudumiwa na Dawasa.
“Suala hili
nililiombea muongozo wa Spika bungeni, Waziri Maghembe akajibu kuwa imeundwa
kamati ya uchunguzi... lakini katika mawasiliano yangu na Naibu Waziri wa
Wizara hiyo, Amos Makalla, alinieleza kuwa uchunguzi umekamilika lakini hakutoa
taarifa hiyo bungeni,” alisema na kuongeza kuwa,
kwa maelezo ya
Makalla, taarifa hiyo ni kwamba ripoti hiyo ya kamati ya uchunguzi tayari
imekwisha kukabidhiwa wizarani kwa ajili ya kuichambua.
“Hivyo ni muda wa
kutosha umepita, nawataka Maghembe na Makalla waiweke taarifa hiyo hadharani
kupitia kwa waandishi wa habari na tovuti ya wizara,” alisema Mnyika na
kuongeza kuwa, pia waeleze hatua walizochukua ikiwemo kuwachukulia hatua
wanaofanya biashara haramu ya maji na kuhujumu miundombinu ya maji, hali ambayo
inawaathiri wananchi.
No comments:
Post a Comment