WAZIRI wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua ripoti ya Utendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira za Mikoa na Miradi ya Kitaifa.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Maji Prof. Jumanne Maghembe amesema Serikali
inadaiwa bilioni 15 na mamlaka za maji nchini.
Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa
ripoti ya utendaji wa mamlaka za maji za mikoa na miradi ya maji kitaifa.
Alisema ukubwa wa deni hilo limekuwa likipunguza uwezo na
ufanisi wa kazi katika mamlaka hizo ikiwemo Dawasco na Dawasa.
"Watu wadogo wadogo ndio ambao wanalipa vizuri bili zao za
maji, lakini mashirika ya serikali hayalipi kabisa, hususani vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama. Dawasco peke yake inaidai serikali bilioni 10.5,
ucheleweshaji wa ulipaji wa deni hili pia unapunguza uwezo wa mamlaka za maji
kununua madawa ya kusafishia maji," alisema.
Maghembe alisema wale wote wanaodaiwa wanatakiwa kulipa madeni
hayo, kwani hali hiyo inahatarisha usalama wa upatikanaji wa maji safi kwa
wananchi.
Aidha alisema moja ya mashirika vinara kwa kupoteza maji ni
Dawasco na Dawasa, ambao hupoteza kwa asilimia 56, hivyo amewataka wabadilike
katika utendaji wao wa kazi na upotevu huo usizidi asilimia 20.
"Mikoa mingine ambayo pia ni vinara kwa upotevu wa maji ni
Mwanza, Bukoba, Arusha. Sasa nataka kuona mabadiliko makubwa na kila mamlaka
ionyeshe inakidhi viwango vya kimataifa kwa kutoa maji safi na salama,"
alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (Ewura), Simon Sayore, alisema ripoti imebainisha kuwa kama
ilivyokuwa mwaka 2012/13, miundo mbinu kwa ajili ya uzalishaji wa maji bado
haitoshelezi mahitaji katika maeneo mengi yanayohudumiwa na mamlaka za maji.
Vile vile alisema ripoti inaonyesha kuwa upotevu wa maji bado ni
tatizo, hivyo wanaamini kwa sehemu kubwa mamlaka za maji zina uwezo wa kuchukua
hatua ili kupunguza tatizo hilo, kwani pamoja na kuhitajika fedha za kukabili nalo,
vile vile uwajibikaji makini wa wafanyakazi wa mamlaka hizo unahitajika.
No comments:
Post a Comment