WANANCHI pamoja na viongozi mbalimbali mkoani Ruvuma wamepokea kwa mshituko na masiktiko msiba wa mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kepteni  John Damiano Komba na kwamba pigo walilolipata ni kubwa hasa kipindi hiki cha Uchaguzi 
Mkuu.

 Baba mdogo wa Kapteni Komba, Fransis Mtokambali alisema alipigiwa simu kutoka Dar-es-salaamu ya taarifa ya msiba ambapo alipigwa na butwaa na kukaa kitambo bila kusema lolote.''Nilipigiwa simu saa moja iliyopita nikiwa nyumbani kwangu Mjimwema Songea na kupewa taarifa ya kifo hiki''alisema.

 Aidha amesema mara moja Kept.Komba aliwahi kusema kuwa ikitokea anakufa azikwe nyumbani kwake Lituhi Nyasa,alisema kama  kauli yake haikutenguliwa wakati amelazwa hospitalini kabla ya kifo chake itabaki kuwa kauli yake ya mwisho ya kuzikwa Lituhi.

 Hata hivyo alisema wanaendelea kufanya mawasiliano na familia ya marehemu iliyopo jijini Dar es Salaam ili kujua utaratibu mzima wa mazishi yake kama yatafanyika Lituhi au Dar es Salaam, baba yake mdogo yupo Lituhi hivyo bado ni mapema kusema mahali atakakozikwa.

 Dereva wa Kapteni Komba (pichani) na rafiki yake wa karibu Hamisi Abdalah Ally walisema walipata taarifa kutoka kwa ndugu mmoja wa marehemu akiwa Dar ambapo hakuiamini hadi alipompigia simu dereva wake Kept. Komba aliyeko Dar es Salaam aliyemtaja kwa jina moja la Hamisi alimhakikishia kuwa ni kweli amefariki dunia.

 Rafiki yake huyo alisema hakuwahi kumsikia Komba akilalamika kama anaumwa ingawa alikuwa anasumbuliwa na kisukali,siku chache zilizopita aliwahi kuambiwa na mtu kuwa Kept.Komba anaumwa baada ya taarifa hiyo hakupata tena taarifa ya ugonjwa wake.

 Meya wa Manispaa ya Songea, Charles Mhagama alisema alipigiwa simu na mtu mmoja kutoka Dar.naye hakuamini alipoambiwa hadi alipoambiwa kuwa mtoa taarifa yupo katika hospitali alikolazwa ya TMJ ndipo alipoamini taarifa hiyo.

 Mhagama alisema kuwa Kept.Komba amekufa wakati ambao anahitajika sana kisiasa na hasa katika jimbo lake la Nyasa kwa kuwa wananchi wake walimzoea licha ya kuwa mhamasishaji mkuu wa chama cha Mapinduzi.

 Naye katibu wa CCM mkoa wa Ruvuma Valena Shumbusho alisema wanachama wa CCM wamepata pigo kubwa lisiloelezeka amewataka kuwa watulivu kipindi hiki chote cha msiba na kuwa na umoja zaidi waweze kumwenzi mpendwa wao kept.Komba.

 ''Hivi hapa ninapoongea nipo mkoani Iringa tumepata msiba wa katibu wetu wa CCM wilaya ya Nyasa Roda tunamzika kesho kabla hatujazika tunapata taarifa ya msiba wa kept.sijui nikuambier nini kuhusu mazishi tusubiri kauri ya viongozi wa chama taifa tukielekezwa tutawafahamisha wananchi''alisema.

 Aliongeza kuwa kwa namna walivyomzoea wananchi wa mkoa wa Ruvuma watamkumbuka sana kwa kazi yake aliyokuwa anaifanya hasa kwa tukio la mwisho la sherehe za CCM kutimiza miaka 38 tangu kuzaliwa kwake zilizofanyika kitaifa Februali 1 uwanja wa Majimaji.

 Shumbusho amewasihi wa wilaya ya Nyasa na mkoa kwa ujumla kuwa wavumilivu wamwombee mbunge wao kwani hili ni pigo ndani ya chama hasa wanapoingia kwenye Uchaguzi Mkuu.