Timu za Ujenzi Rukwa na Volcano FC ya Morogoro zimeshushwa
madaraja mawili hadi ligi za wilaya baada ya kushindwa kufika uwanjani kwenye
mechi zao za Ligi Daraja la Pili (SDL).
Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana jijini Dar es Salaam kupitia
ripoti za matukio mbalimbali ya ligi hiyo.
Ujenzi Rukwa ilishindwa kwenda Kigoma kuikabili Mvuvumwa FC
ya huko wakati Volcano FC haikutokea kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine
jijini Mbeya ambapo ilitakiwa kucheza na Wenda FC.
Uamuzi wa Kamati ya Mashindano umefanywa kwa kuzingatia
Kanuni ya 27 ya SDL ambapo mbali ya kushushwa madaraja mawili, lakini pia timu
hizo zimepigwa faini ya sh. milioni moja kila moja. Vilevile matokeo yote ya
mechi zao kwenye Ligi hiyo yamefutwa.
Nayo Singida United imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao
matatu baada ya Ujenzi Rukwa kubainika kumchezesha mchezaji asiyestahili (non
qualified) kwenye mechi iliofanyika Februari 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa
Mandela mjini Sumbawanga na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.
Mchezaji Emmanuel Elias Mseja wa Mbao FC amepigwa faini ya
sh. 100,000 na kufungiwa mechi tatu baada ya kukojoa uwanjani kwenye mechi
dhidi ya AFC iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid
jijini Arusha.
Pia viongozi wa Mbao FC, Abdallah Chuma (Daktari) na Meneja
Yasin Abdul wamefungiwa miezi sita na faini ya sh. 100,000 kila mmoja kwa
kumtukana na kumtishia maisha Kamishna wa mechi hiyo.
Nayo klabu ya AFC imepigwa faini ya sh. 300,000 kutokana na
washabiki wake kuifanyia vurugu timu ya Bulyanhulu FC kwenye mechi yao
iliyofanyika Februari 7 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri
Abeid na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Timu ya Magereza Iringa imepigwa faini ya jumla ya sh.
200,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match
meeting), na uwanjani kwenye mchezo wao na Njombe Mji uliochezwa Februari 21
mwaka huu. Naye mchezaji wa timu Amasha Mlowasa amefungiwa mechi tatu na faini
ya sh. 100,000 kwa kumtukana mchezaji mwenzake kwenye mechi hiyo.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment