NA BRYCESON MATHIAS, DODOMA
MSAIDIZI wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania Dayosisi ya Dodoma, Samwel Mshana, amekemea vikali na kuwaonya waandaaji
wa Tamasha la Tangaza Amani, Imba na Badilisha Kipato kuwa Ajira, kwamba
kanisani si mahali pa biashara bali ni nyumba ya ibada.
Askofu Mshana alisema hayo Jumatatu, Aprili 6, kwenye
Pasaka ya Pili, ambapo kwenye Tamasha la Uimbaji wa Kwaya mbalimbali
lililoandaliwa na RASI FM Radio yenye masafa ya 103:7 FM, kwenye ratiba yao
waliweka tukio la kukata keki ya biashara (pichani) yenye umbo la kanisa.
Keki yenye umbo la Kanisa iliyokusudiwa iuzwe
kanisani KKKT, Usharika wa Kanisa Kuu Dodoma, ambapo Msaidizi wa Askofu, ambaye
ndiye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Samwel Mshana, alikataa kanisa lake
kufanywa mahali pa biashara.
Akifungua tamasha hilo kwenye Kanisa Kuu la KKKT Dodoma,
Askofu Mshana, ambaye ndiye Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo, ili kulinda maadili
ya kanisa, aliwajia juu waandaaji hao akisema ana mambo matatu ambayo
hayakumfurahisha wanayotakiwa kuyakomesha mara moja.
“Waandaaji mmeshindwa kuzingatia muda, mlisema tamasha
litaanza saa sita mchana na mimi askofu nitafungua tamasha hilo saa tisa
(15:10-15:40), lakini hadi saa nane hii ndiyo kwanza mnaanza, ikiwa hivyo, siku
nyingine msiniite, sitakuja!
“Kwenye ratiba yenu kipengele cha tisa, mmeonyesha kuna kukata
keki ya biashara, napenda niwaonye kanisani si mahali pa biashara, hivyo sitaki
kuona kwenye Kanisa lolote la KKKT Dodoma ninaloliongoza kunafanywa biashara, kama
kuna biashara hiyo ikafanyiwe nje ya kanisa,” alikemea Mshana.
Alionya kuwa kanisa ni mahali pa kusifu na kuabudu; ni nyumba
ya ibada, ambapo watu wanaomba, wanaimba na kuponywa magonjwa, huzuni na taabu
zao, ili wapate furaha na kuhuishwa uhai wa kiroho na miili yao! Lakini
katu si mahali pa kufanya biashara.
Alisema tunasoma katika Luka 19:45; “(Yesu); Akaingia
hekaluni akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, imeandikwa,
nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; Lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.
Msifanye hivyo hapa!
Baada ya Kiongozi wa uandaaji wa tamasha hilo kukiri kuwepo
makosa ya uchapaji na kwamba tukio hilo halitafanyika, Askofu Mshana alifungua uimbaji
huo akiwataka waimbaji wawe kama mwanamke, Mariamu Magadalene, ambaye alijua
umuhimu wa Kanisa na Yesu, aliyemponya, kiasi cha kufika kaburini alipozikwa ili
ampake manukato.
Waumini na wadau wa habari, walishangazwa na waandaji hao
ambao ni wanahabari, kushindwa kujali muda, jambo ambalo ni kubwa na muhimu
katika fani ya kazi yao ili kuweza kuwahi matukio ya uandishi wa habari za radio,
TV na magazeti.
Keki yenye umbo la Kanisa la iliyokusudiwa iuzwe kanisani KKKT Usharika
wa Kanisa Kuu Dodoma, ambapo Msaidi wa Askofu ambaye ndiye Mchungaji Kiongozi
wa Kanisa hilo Samwel Mshana alikata Kanisa lake kufanywa mahali pa Biashara.
No comments:
Post a Comment