Kufuatia mchezaji Mbwana Samatta kushinda tuzo ya mchezaji bora wa
Afrika kwa wachezaji wa ndani, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) lilikuwa limeandaa shughuli maalum ya kumpongeza, kumshukuru na
kumtakia kheri katika taaluma yake ya uchezaji mpira.
Kama ilivyotangazwa hapo awali shughuli hii ilikuwa ifanyike kesho
Alhamisi tarehe 14/01/2016 Makao Makuu ya TFF Uwanja wa Karume kuanzia
saa 11 jioni.
Tarehe hii ilipangwa mahsusi ili kupisha shughuli za kitaifa za siku
ya Mapinduzi tarehe 12/01/2016 na fainali ya Kombe la Mapinduzi tarehe
13/01/2016.
Kufuatia maandalizi ya Mbwana Samatta ya safari ya kuelekea Ulaya
kukamilika hivyo mchezaji huyo siku ya Alhamisi hatoweza kuhudhuria
shughuli hii na hivyo shughuli haitakuwepo tena.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea tena
kumpongeza Mbwana Samatta kwa mafanikio aliyoyapata na pia kumtaka huko
aendako aendelee kuwa mfano mwema kwa vijana wote wa Tanzania.
TFF inamshukuru sana Mh Rais John Pombe Magufuli kwa salamu za
pongezi alizozitoa kufuatia ushindi wa Mbwana, Wanafamilia wa Mpira wa
Miguu tumefarijika sana kwa salam hizi.
Tunamshukuru sana Waziri Mkuu Mh Majaliwa Kassim Majaliwa kwa
kumuandalia jana Mbwana Samatta hafla katika hoteli ya Hyatt na kwa
kumpatia zawadi zikiwemo fedha taslim na kiwanja eneo la Kigamboni.
Tunamshukuru sana Mh Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
Sanaa na Michezo pamoja na viongozi wote wa Wizara kwa kujitolea kwao
kushiriki katika shughuli mbalimbali za kumpokea na kumpongeza Mbwana
Samatta.
Shukrani za pekee pia kwa wazazi wake Mbwana Samatta, pia familia na washauri wake.
No comments:
Post a Comment