NIMESOMA andishi la anayejiita Seif Rashid, lililochapishwa
kwenye mitandao kadhaa ya kijamii, pamoja na baadhi ya magazeti.
Andishi limejielekeza katika kunijadili binafsi: Jinsi
nilivyofanikiwa kuwa mbunge wa jimbo la Ubungo, kuwa mmiliki wa kampuni ya Hali
Halisi Publishers Limited – wachapishaji
wa MwanaHALISI – gazeti ambalo mimi ndiye mtendaji wake mkuu – na mengine
mengi.
Andishi hili lilipewa vichwa vya maneno tofauti, kulingana
na mahitaji ya mchapishaji.
Kuna baadhi ya maeneo lilipewa kichwa cha maneno, “Saed
Kubenea: Ndumilakuwili mbobezi.” Pengine ililiandikwa, “Mfahamu Saed Kubenea,
mbunge wa Ubungo.”
Kote lilikochapishwa andishi lile, lilibeba aya kadhaa
kutoka kwenye makala niliyoandika na kuchapishwa katika gazeti la MAWIO, toleo
la Alhamisi ya 24 Desemba 2015.
Makala katika MAWIO ilikuwa inajadili ndimi mbili za
Kiongozi Mkuu wa ACT- Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe.
Mwandishi anasema, nimeamua kumshambulia Zitto, kwa sababu
nataka kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo
Zitto pia anaitaka tena.
Baada ya kuisoma na kuirejea tena na tena, napenda kueleza
yafuatayo:
Ni kweli kwamba Saed Kubenea ndilo jina langu. Ni kweli kuwa
mimi ni mbunge wa Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Ni kweli kwamba niliwahi kuandikia magazeti ya Mtanzania na RAI – hakuna lililo
la kweli. Basi. Yaliyobaki katika andishi la anayejiita Seif Rashid, ni uongo
wa moja kwa moja, porojo au tuhuma zenye nia ya kunidhalilisha na kunivunja
moyo.
Niseme hapa mapema kuwa, mimi siyo mtu wa kuvunjika moyo
pale ninapokuwa nimeamua kufanya jambo. Mimi sitishwi na uongo, uzushi, porojo
au suto za kwenye magenge ya kahawa au bao.
Alichokifanya anayejiita Seif Rashid, ni kuokoteza huku na
kule na kutaka kuaminisha umma kuwa ni ukweli. Kwa mfano, sijawahi kutamka
mahali kokote kuwa nataka kuwa mwenyekiti wa PAC.
Spika wa Bunge hajapanga nani awe kamati hii au ile. Wala haijafahamika kuwa
nitakuwa mjumbe wa kamati ipi.
Hata kama nitataka kuwa mwenyekiti, bado siwezi kutumia
kalamu yangu kujipigia kampeni. Siamini katika siasa za aina hiyo.
Mwenye andishi anasema, ninatumia cheti cha ndugu yangu
aishiye Bagamoyo na mwenye jina la Said (sio Saed); na kwamba mimi siitwi Saed
Kubenea. Hataji jina langu.
Hata hivyo, ni vema nieleze yafuatayo: Jina la Saed Kubenea,
ndiyo jina halisi nililopewa na wazazi wangu. Nimelirithi kutoka kwa babu
yangu. Anaitwa, Saed Mohammed Kubenea. Aidha, hakuna kaka au ndugu yangu yeyote
anayeishi Bagamoyo. Hayupo.
Nimesoma kwa kadri Mwenyezi Mungu alivyonisaidia. Nilimaliza
Kidato cha Nne. Nikaanza kujifunza mwenyewe na baadaye kupata msaada wa watu
mahili kunifundisha taratibu uandishi wa habari. Nikahudhuria mafunzo mafupi
hapa na pale nchini. Hatimaye nikapata mafunzo ya juu ya uandishi wa habari
nchini Uholanzi na India.
Ninaendelea kujifunza na elimu haina mwisho.
Jingine la kugusia ni madai kuwa nilihusika na upoteaji wa
anachoita, “kompyuta mpakato (laptop) ya Prof. Ibrahim Lipumba mwaka 2005.”
Suala hili liliwahi kuelezwa pia na Didas Masaburi,
aliyekuwa mshindani wangu katika mbio za ubunge jimboni Ubungo.
Ukweli ni huu: Prof. Lipumba hajawahi kuibiwa kompyuta
(laptop) akiwa na mimi. Kilichoibiwa akiwa na mimi ni modemu inayotumika kwa
ajili ya kupata huduma ya intaneti. Bali kompyuta inayodaiwa kuwa ya Prof.
Lipumba ilikuwa ni mali
yangu. Siyo ya Prof. Lipumba kama ambavyo
wahusika wanataka kuaminisha umma.
Kuna hili la gazeti la Hali Halisi ambalo mwandishi anasema,
nilipewa mtaji na Prof. Lipumba na baadaye likatumika kama
gazeti rasmi la kambi ya upinzani bungeni. Mimi sikuanzisha gazeti hili.
Lilianzishwa na wabunge wa upinzani mwaka 2003. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
alikuwa Willifred Lwakatare, mbunge wa Bukoba Mjini wakati huo.
Ninashangaa mtuhumu anapopata taarifa kwamba kufa kwa gazeti
la Hali Halisi, kulinifanya kuwa na maisha magumu; na kwamba kwa huruma, Zitto Kabwe na mwenzake, Halima
Mdee, wakanipa mtaji wa kuanzisha gazeti la MwanaHALISI. Hii siyo kweli na
aliyeandika hivyo anajua si kweli.
Kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited ilianzishwa 31
Januari 2005. Wakati huo Zitto na Mdee hawakuwa wabunge. Zitto na Halima
hawakushiriki kwa namna yoyote ile katika kuanzisha gazeti hili. Mdee akiulizwa
juu ya hili ataeleza. Hata Zitto anajua vema; na akiwa mkweli, atasema
hivyohivyo. Historia isipotoshwe.
Gazeti la MwanaHALISI limeanzishwa na mimi kwa ushirikiano
mkubwa kutoka kwa Absalom Kibanda na baadhi ya waandishi wengine mahiri. Labda
niseme hivi, kwamba anayetaka kujua historia yangu, ya vyombo vyangu vya habari
na maisha yangu ya mapambano; afanye ahadi na mimi, tukae, aniulize, nimweleze
ili apate ukweli na usahihi juu yangu na kazi yangu, na hata ubunge wangu.
Hebu niweke wazi jambo hili: Kwanza,
sijawahi kuwa na urafiki, kwa maana halisi ya urafiki, na Zitto. Kilichokuwepo
ni ukaribu tu kama ilivyo kwa watu wengine
mnapokuwa pamoja.
Pili, sishindani na Zitto. Katika lipi? Kila mmoja ana
taaluma yake; na taaluma hizi zaweza kufanya kazi nzuri na vizuri kama
hakutakuwa na unafiki, uzandiki na undumila kuwili kama
nilioueleza katika makala yangu.
Tatu, siamini katika kuomba fadhila na kujikomba. Naamini
katika kudai haki na kilichochangu; au ninachostahili kwa mujibu wa taratibu,
kanuni, sheria na katiba. Haya hayahitahi kujikomba. Yanahitaji ujasiri na moyo
wa utumishi kwa umma. Huko ndiko kwangu.
Saed Kubenea.
No comments:
Post a Comment