Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo wakati akitangaza kufutwa kwa gazeti la Mawio. (Picha na Habari Mseto Blog)
DAR ES SALAAM, TANZANIA
Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania imeamua kulifuta kutoka katika Daftari la usajili wa
magazeti, gazeti lijulikanalo kama “MAWIO”.
Amri ya kulifuta Gazeti hilo imetolewa kwa Tangazo la Serikali Na. 55 lililotolewa
tarehe 15 Januari, 2016. Uamuzi huo umetolewa kwa mjibu wa Sheria ya Magazeti Sura
ya 229, kifungu 25(1).
Hatua hii pia
inazuia gazeti la Mawio kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja
na mitandao (Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya
Kieletroniki na Posta Sura ya 306.
Serikali kwa
masikitiko makubwa, imechukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa
gazeti hilo usioridhisha wa kuandika na kuchapisha habari zenye mwelekeo wa
uchochezi na kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi yetu.
Aidha, hatua hii ya
kulifuta gazeti hilo imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi
kubwa za muda mrefu kuanzia Juni, 2013 hadi Januari, 2016 kumtaka Mhariri wa gazeti hilo kubadili aina
ya uandishi wa habari na makala katika gazeti lake, bila mafanikio.
Msajili wa magazeti
kwa juhudi zake alifanya mawasiliano na mhariri wa gazeti hilo mara nane kwa
lengo la kutaka afanye marekebisho ya mtindo wa kutoa habari zake lakini mhariri wa
gazeti hilo hakuzingatia ushauri mzuri aliopewa na Msajili wa Magazeti.
Ninatoa wito kwa
wamiliki, wahariri, waandishi na watangazaji wa habari kuzingatia sheria,
Kanuni na taratibu za taaluma ya uandishi wa habari ambazo zikizingatiwa
hakutakuwa na migogoro yoyote. Aidha Serikali inasisitiza kwamba inaheshimu
uhuru wa vyombo vya habari unaozingatia maadili, weledi na Sheria za nchi na
kwamba Serikali itaendelea kushirikiana navyo
Kwa upande mwingine
ninatoa pongezi kwa vyombo vyote vya habari nchini vinavyozingatia maadili,
weledi na Sheria zinazosimamia taaluma ya habari na sheria nyingine za nchi. Kwa namna ya pekee Serikali inawapongeza
wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari ambavyo vinapofanya makosa
vikielekezwa hujirekebisha na kutoa ushirikiano kwa Serikali na pia kubadili
mwenendo wao; hawa ni pamoja na wahariri
wa magazeti ya;
·
Mwananchi Tanzania
·
Mtanzania
·
The East African
·
Magazeti ya Daily News na Habari Leo
·
Uhuru na mengineyo
Ninapenda kusisitiza kwamba Serikali inapenda kujenga
uhusiano mzuri na wa kirafiki kati yake na wadau wa sekta ya habari. Aidha ninasisitiza
tena wadau wa sekta hii kuzingatia Sheria ili kujenga heshima ya tasnia ya
habari na kulinda amani ya nchi yetu.
Imetolewa na Nape M. Nnauye (Mb,)
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Dar es Salaam, leo tarehe 17
Januari, 2016
No comments:
Post a Comment