KAMATI
ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka imewatangaza waimbaji wengine
watakaopanda jukwaa la tamasha hilo linalotarajia kufanyika mikoa ya
Geita, Mwanza na Wilaya ya Kahama ikiwa ni muendelezo wa maandalizi ya
kuelekea sikukuu hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya
maandalizi, Alex Msama wameongeza idadi ya waimbaji katika tamasha hilo
ambao ni Christopher Mwahangila na Joshua Mlelwa.
Msama alisema
wamepanga tamasha hilo litakaloanza Machi 26 mkoani Geita kwenye ukumbi
wa Desire huku Machi 27 litafanyika jijini Mwanza katika uwanja wa CCM
Kirumba na Machi 28 litamalizia Uwanja wa Taifa ulioko Wilayani Kahama.
Msama
alitumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi
ili kufanikisha malengo ya tamasha hilo ambayo ni pamoja na kusaidia
wenye uhitaji maalum kama yatima, walemavu na wajane.
Aidha Msama alisema mwaka huu kamati yake imejipanga kugawa baiskeli zaidi ya 100 kwa walemavu ikiwa ni sehemu ya tamasha hilo.
"Tamasha
la Pasaka linawajali wenye uhitaji maalum kama walemavu, yatima na
wajane ambao wanapata misaada kupitia mapato ya mlangoni kupitia
viingilio," alisema Msama.
Msama aliwataja waimbaji wengine
waliothibitisha kushiriki tamasha hilo ni pamoja na Rose Muhando, Bonny
Mwaitege, Upendo Nkone, Jesca BM Honore, Faustine Munishi, Anastazia
Mukabwa na Jennifer Mgendi.
No comments:
Post a Comment