Baraza la Michezo Tanzania (BMT), limebariki Uchaguzi Mkuu wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likisema: “Tunaitakia TFF uchaguzi
mwema wenye amani, upendo na utulivu.”
Pamoja na baraka hizo, Baraza limeiagiza TFF kuwaelekeza
wagombea wote kuzipitia sheria za Baraza la Michezo, Kanuni za Baraza na kanuni
za Usajili, hususani kanuni ya 8 (1) na (2).
Kanuni hiyo ya 8 (1) na (2), inaagiza kuwa endapo wagombea wote
watakaoshinda nafasi wanazowania kwa sasa ndani ya TFF, hawana budi kuachia
nafasi mojawapo katika uongozi wa mpira kwa miguu katika ngazi ya wilaya au
mkoa aliyoshinda awali.
BMT imetoa agizo hilo ikiwa ni kukumbushana juu ya utii wa
sheria na kuepuka kushika nyadhifa mbili kwa wakati mmoja.
Katika barua yake iliyoandikwa Juni 19, mwaka huu na kusainiwa
na Katibu Mkuu wa BMT, Mohammed Kiganja, Baraza hilo limesema: “Uchaguzi huu
usivuruge amani iliyopo nchini. Wagombea wakumbuke kuwa kuna maisha baada ya
uchaguzi.”
Baraza limesisitiza kuwepo na haki katika mchakato mzima
kuelekea kwenye uchaguzi. Uchaguzi na mchakato wake uwe huru na amani na usiwe
ni kichocheo cha uvunjifu wa amani.
Baada ya viongozi kupatikana, watakula kiapo cha utii, na kujaza
fomu Namba 5 ya BMT ya utekelezaji majukumu yao kama Kanuni ya 8 (4)
inavyoeleza.
Kadhalika, mara baada ya uchaguzi, Baraza limeagiza kuhusisha
baadhi ya vifungu vya sheria ya Baraza ili viendane na katiba za TFF na wadau
pamoja na kanuni zao.
……………………………………………………………………………… ………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA
MIGUU TANZANIA
No comments:
Post a Comment