HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 21, 2017

MAKAMU WA RAIS AKABIDHI VIFAA VYA KUSAIDIA WAKINA MAMA WAJAWAZITO WAKATI WA KUJIFUNGUA KATIKA HOSPITALI MBILI MBAGALA


  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa hafla maalum ya kukabidhi vifaa vya kusaidia wakina mama wajawazito wakati na baada ya kujifungua vilivyotolewa na Shirika la Red Crescent la Kuwait ambapo mabeseni 100 yenye vifaa hivyo kati ya 1000 yalikabidhiwa kwa hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, Dar Es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia mabeseni yaliosheheni vifaa vya kuwasaidia wajawazito wakati wa kujifungua pamoja na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Jasem Al-Najem kwenye  hafla maalum ya kukabidhi vifaa vya kusaidia wakina mama wajawazito wakati na baada ya kujifungua vilivyotolewa na Shirika la Red Crescent la Kuwait ambapo mabeseni 100 yenye vifaa hivyo kati ya 1000 yalikabidhiwa kwa hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, pia vifaa hivyo viligawiwa pia katika kituo cha Afya cha Mbagala Round Table kilichopo Mbagala Kizuiani.
 Wananchi waliohudhulia hafla hiyo.

Dar es Salaam, Tanzania. 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amezindua zoezi la ugawaji wa mabeseni yenye vifaa tiba 200 yaliyotolewa na Ubalozi wa Kuwait nchini kwa ajili ya wanawake wajawazito katika hospitali ya Mbagala Zakiem na Kituo cha Afya cha Mbagala Round Table katika wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam.


Lengo la mpango huo ni kutoa mabeseni hayo zaidi ya 1,000 kwa wanawake wajawazito wasio na uwezo kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar kama hatua ya kukabiliana na vifo vya watoto na wanawake wajawazito nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vifaa tiba hivyo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa mpango huo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupambana na vifo vya watoto na wanawake wajawazito kwa kukosa vifaa tiba kutokana na umaskini unaowakabili.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kwa maeneo yaliyopatiwa mabeseni yenye vifaa tiba yahakikishe vifaa hivyo vinatolewa kwa wanawake wajawazito ambao baadhi yao wanakata tamaa kwenda kujifungulia kwenye hospitali au kwenye vituo vya afya  kwa kukosa vifaa hivyo kwa sababu ya umaskini.

Amesema mkakati uliopo wa Serikali ni kuhakikisha huduma za afya nchini zinaendelea kuboreshwa hasa huduma ya mama na mtoto ambapo kutokana na umuhimu wa sekta ya afya Serikali imetenga fedha za kutoka katika bajeti ya mwaka 2017/2018.

Makamu wa Rais ameeleza kuwa mradi huo wa ugawaji wa mabeseni yenye vifaa tiba katika mradi huo kuanzia sasa utasimamia na wake wa viongozi wastaafu na wakiwemo wake wa mawaziri baada ya kuuzindua rasmi.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia ameishukuru Serikali ya Kuwait kwa msaada wake huo ambao amesema utakuwa ni chachu ya kupambana na vifo vya watoto na wanawake wajawazito Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa upande wake, Balozi wa Kuwait hapa nchini Jasem Al- Najem amesema Serikali ya Kuwait kupitia kwa Jumuiya ya Red Crescent ya nchini hiyo itaendelea kusaidia vifaa tiba mbalimbali kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo yao.

Balozi huyo wa Kuwait hapa nchini Jasem Al- Najem amesisitiza kuwa milango ya ubalozi wa Kuwait ipo wazi kwa Taasisi mbalimbali za Kiserikali kupeleka maandiko mbalimbali kwa ajili ya kuomba kupatiwa misaada lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma za viwango vya juu katika sekta mbalimbali.

Amesema kwa sasa Serikali ya Kuwait ipo mbioni kutiliana saini ya makubaliano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Unguja.

Ameeleza kuwa ukarabati huo utaiwezesha hospitali hiyo kuongeza utoaji wa huduma bora kwa wananchi wengi zaidi.

Halfa ya makabidhiano ya mabeseni 200 ya vifaa tiba katika hospitali ya Mbagala Zakiem na Kituo cha Afya cha Mbagala Round Table katika wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages