WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inayatambua na kuyathamini mahusiano mazuri ya kidiplomasia yaliyojengwa na awamu zilizotangulia baina ya Tanzania na mataifa mbalimbali ikiwemo Jamuhuri ya Cuba na kwamba itayaendelea.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Agosti 17, 2017), alipozungumza
na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Bi Anna Teressa mara baada ya kuwasili
nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye
lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
“Tanzania na Cuba zina historia ya kutosha. Tunatambua mahusiano
mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya
Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere.”
Amesema katika ziara yake hiyo anatarajia kufanya mazungumzo na
viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali ya Cuba kwa lengo la kukuza
ushirikiano katika sekta za Afya, Elimu, Utalii na Kilimo.
Waziri Mkuu amesema Cuba ni mojawapo kati ya nchi zenye
ushirikano wa muda mrefu na Tanzania kisiasa, kijamii, kiafya na kiuchumi.”Mfano
katika Sekta ya Afya, madaktari wengi kutoka Cuba walikuwa wanakuja Tanzania
kutibu wagonja waliokuwa na maradhi makubwa.”
Pia
Waziri Mkuu amesema katika ziara hiyo anatarajia kukutana na Jumuya ya
Wafanyabiashara wa Cuba ili kuwaelezea fursa za uwekezaji zilizopo nchini
Tanzania hususan katika Sekta ya Viwanda
pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Kwa upande wake Bi. Anna ambaye alimpokea Waziri Mkuu kwa niaba ya
Serikali ya Cuba alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa
kuendelea ushirikiano mzuri baina ya nchi hizo mbili, hivyo alimuhakikishia
kwamba wataendelea kuudumisha.
Pia
Bi. Anna ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa namna inavyopambana na rushwa, ufisadi,
kuhimiza uwajibikaji pamoja na kutetea wanyonge.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 18, 2017.
No comments:
Post a Comment