WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inayatambua na kuyathamini mahusiano mazuri ya kidiplomasia yaliyojengwa na awamu zilizotangulia baina ya Tanzania na mataifa mbalimbali ikiwemo Jamuhuri ya Cuba na kwamba itayaendelea.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Agosti 17, 2017), alipozungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Bi Anna Teressa mara baada ya kuwasili nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
“Tanzania
na Cuba zina historia ya kutosha. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo
kati nchi zote mbili, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya
kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere.”
Amesema
katika ziara yake hiyo anatarajia kufanya mazungumzo na viongozi
mbalimbali waandamizi wa Serikali ya Cuba kwa lengo la kukuza
ushirikiano katika sekta za Afya, Elimu, Utalii na Kilimo.
Waziri
Mkuu amesema Cuba ni mojawapo kati ya nchi zenye ushirikano wa muda
mrefu na Tanzania kisiasa, kijamii, kiafya na kiuchumi.”Mfano katika
Sekta ya Afya, madaktari wengi kutoka Cuba walikuwa wanakuja Tanzania
kutibu wagonja waliokuwa na maradhi makubwa.”
Pia
Waziri Mkuu amesema katika ziara hiyo anatarajia kukutana na Jumuya ya
Wafanyabiashara wa Cuba ili kuwaelezea fursa za uwekezaji zilizopo
nchini Tanzania hususan katika Sekta ya Viwanda pamoja na kutangaza
vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Kwa upande wake Bi.
Anna ambaye alimpokea Waziri Mkuu kwa niaba ya Serikali ya Cuba
alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea
ushirikiano mzuri baina ya nchi hizo mbili, hivyo alimuhakikishia kwamba
wataendelea kuudumisha.
Pia
Bi. Anna ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya
Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa namna inavyopambana na
rushwa, ufisadi, kuhimiza uwajibikaji pamoja na kutetea wanyonge.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 18, 2017.
No comments:
Post a Comment