*Ataka waache kutoa hovyo vibali vya uvunaji misitu
*Ahimiza utunzaji misitu, mazingira
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya kutoa
vibali vya uvunaji mbao inayofanywa na maafisa misitu wa TFS ambao wako
chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Ametoa onyo hilo leo mchana (Jumamosi, Agosti 12,
2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye
mkutano uliofanyika kata ya Goweko, wilayani Uyui mkoani Tabora.
Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada ya kumhoji
Afisa Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Juma Kazimoto na
Afisa Misitu wa Wilaya, Bw. Jared Nzilorera na kubaini kuwa hawafanyi kazi kwa
kushirikiana.
"Hapa kuna uvunaji mkubwa wa misitu. Je kuna
mtu anafuatilia kama wanavuna kwa usahihi?" alihoji Waziri Mkuu.
Akijibu swali la Waziri Mkuu, Bw. Kazimoto
alisema Uyui hakuna uvunaji lakini wanaovuna wanatoka Sikonge na kuja kuuza
mbao Uyui.
Alipoulizwa Afisa Misitu wa Wilaya, ni kwa
kiasi gani wanapeana taarifa na mwenzake wa TFS ambao wanaletwa na wizara,
alitoa majibu ya kujichanganya hali iliyomfanya Waziri Mkuu aamue kukemea tabia
yao ya kutoa vibali bila kuwahusisha wenzao wa Halmashauri.
"TFS mmejiingiza kwenye kuvuna misitu, na
mnawaover-power DFOs (wale wa Halmashauri). Hawa walioko kwenye Halmashauri
ndiyo wanaolinda misitu yote ambayo iko ndani ya wilaya husika."
"Tatizo hili liko nchi nzima, ni la ushindani
kati ya maafisa misitu wa TFS na wale wa Halmashauri. Misitu yetu inakwisha
sababu mnaimaliza nyie kwa kutoa vibali bila kuwashirikisha wenzenu.
Alimwagiza Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Bi. Queen
Mlozi asimamie suala hilo. "DC wewe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya, simamia jambo hili na usisitize utunzaji wa mazingira na
upandaji miti," alisema.
Alisema ukataji miti ovyo umechangia kukauka kwa
vyanzo vingi vya maji. "Mhandisi wa Maji anahangaika kuchimba visima
lakini hakuti maji sababu miti imekatwa ovyo na ardhi tepetevu imekauka.
Watumishi wote nendeni vijijini mkahamasishe utunzaji wa mazingira," alisema.
Kwa mujibu wa hali ilivyo sasa, kila mkoa una
Afisa Misitu wa Mkoa, kila wilaya imeajiri Afisa Misitu wa Halmashauri, lakini
Wizara pia imeajiri Maafisa wa Misitu kutoka TFS katika ngazi za mkoa na
wilaya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, AGOSTI 12, 2017.
No comments:
Post a Comment