WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wanaoishi
kwenye makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu waache kujihusisha na matukio ya
uhalifu.
Ametoa onyo hilo leo mchana (Ijumaa, Agosti 11,
2017) wakati akiwahutubia mamia ya wakazi wa tarafa ya Ulyankulu katika mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya VETA, wilayani Kaliua mkoani
Tabora.
Amesema matukio ya ujambazi, mauaji na umiliki wa
silaha yanayofanyika kwenye tarafa hiyo ni mengi ikilinganishwa hali ilivyo
kwenye maeneo mengine ya mkoa huo.
"Taarifa nilizonazo zinaonyesha katika kipindi
cha miaka miwili kumekuwa na matukio ya mauaji 35, ujambazi matukio 12, umiliki
wa silaha nao unatisha. Yamekamatwa magobole 11, bunduki aina ya SMG saba na Mark Four mbili."
"Tulikamata pia risasi 714 za SMG zikiwa
kwenye ndoo za mafuta na juu yake wamepaka mafuta ya mawese. Pia risasi mbili
za Mark Four zilikamatwa," amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amewataka wakazi hao ambao baadhi yao
wamepewa uraia na wengine bado ni wakimbizi waonyane wanapokutana kwenye vikao
vyao kwa sababu matendo yao yanaikwaza Serikali ambayo iliamua kuwapa hifadhi.
"Ni vema mkikutana kwenye vikao vyenu muelezane na kuonyana," amesema
Waziri Mkuu.
"Ninawasihi matukio haya myadhibiti la sivyo
mtaharibu nia njema iliyoleta uwepo wenu. Bunduki na risasi zinakuja
kufanya nini wakati nyie mko maeneo salama? Mauaji ya nini? Kama kuna
tatizo limekupata, muone mwenyekiti wa kijiji, atakusaidia,"
alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi yao ambao
wamegeuka mawakala na wameanza kuwaleta ndugu zao bila kufuata utaratibu.
"Hatuzuii mtu kutembelewa na ndugu yake, lakini ni lazima mfuate taratibu.
Tunataka tudumishe amani iliyopo nchini lakini pia tudumishe urafiki wa nchi
zetu mbili za Burundi na Tanzania," aliongeza.
Mapema, Mbunge wa jimbo la Ulyankulu, Bw. John Kadutu alimuomba Waziri Mkuu
afuatilie suala la upatikanaji wa maji kwenye tarafa hiyo, pia aliomba
wasaidiwe ili kata tatu za Kanindo, Igombenkulu na Milambo ziwezeshwe kufanya
uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 11, 2017.
No comments:
Post a Comment