WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Viwanda vya Sukari nchini Cuba, Bw. Francisco Lled, ambaye amekubali kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.
Shirika
la Sukari la nchini Cuba linauwezo wa kuzalisha tani milioni nne za sukati kwa
mwaka huku mahitaji ya ndani ni tani 700,000, ambapo kiasi kinachobaki huuzwa
nje ya nchi. Kwa sasa shirika hilo linazalisha tani milioni mbili tu katika
viwanda vyake 56.
Waziri
Mkuu alikutana na Bw. Lled jana (Alhamisi, Agosti 24, 2017), wakati alipofanya
ziara katika kiwanda cha kuzalisha sukari cha UGB Central Azucarero 30 de
Noviembre katika mji wa San Nicola’s de Bari ambacho ni kati ya viwanda 27 vya shirika
hilo linalomilikiwa na Serikali ya Cuba kwa asilimia 100.
Katika
mazungumzo yao Waziri Mkuu alimshawishi Bw. Lled
kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha sukari.
Alisema kwa sasa Tanzania kuna viwanda vikubwa vitano vya sukari ambavyo
uzalishaji wake hautoshelezi mahitaji ya ndani.
Waziri
Mkuu alivitaja viwanda hivyo ambavyo ni Mtibwa na Kilombero (Morogoro), Mahonda
(Zanzibar), TPC (Kilimanjaro) na Kagera
ambavyo vyote vinazalisha jumla ya tani 320,000 za sukari kwa mwaka huku
mahitaji yakiwa ni zaidi ya tani 400,000.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi
inatarajia kujenga viwanda vitatu vya kuzalisha sukari, ambavyo vitazalisha
sukari itakayotosheleza mahitaji na ndani ya nchi na kiasi kitakachosalia
kitauzwa nje.
Kwa upande wake Bw. Lled alisema sera za Cuba haziruhusu shirika kwenda kuwekeza nje
ya nchi na badala yake wanaruhusiwa kuzisaidia nchi zinazohitaji kujenga
viwanda hivyo kwa kutoa ushauri na usimamizi wa ujenzi wa miradi hiyo.
Alisema
Shirika lake lipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika usimamizi
na kutoa ushauri wa ujenzi wa miradi ya viwanda vya kuzalisha sukari na kwamba
walishatoa huduma kama hiyo katika nchi mbalimbali zikiwemo Brazil na Bolivia.
Katika
hatua nyingine, Bw. Lled alisema mbali na uzalishaji sukari pia shirika hilo
kupitia viwanda vyake vya sukari wanazalisha vyakula vya mifugo, asali ambayo
inatumika katika viwanda vya kutengeneza vinywaji vikali pamoja nishati ya
umeme.
Alisema
miwa ya kuzalishia sukari katika viwanda vyao wanaipata kutoka kwenye vikundi
vya ushirika wa kulima wa miwa vilivyoko katika mikoa yote nchi nzima kasoro
mkoa wa Havana na Pañar del Rio na kwa mkulima mmoja mmoja ambao kwa pamoja hukusanya
miwa katika vituo ambavyo hupeleka kiwandani.
Hata
hivyo alisema kuwa viwanda vyao vinanunua miwa kwa bei tofauti kulingana na ubora
wa miwa na kwamba shirika lao linawasaidia wakulima kwa kuwaelimisha namna bora
ya kulima pamoja na kuwaazima mashine za kuvunia wakati wa mavuno. Miwa yote
nchini Cuba inavunwa kwa kutumia mashine.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAAA, AGOSTI 25, 2017.
No comments:
Post a Comment