HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 16, 2017

WAHITIMU TIA WAMEASWA KUJIHUSISHA NA UBADHIRIFU WA MALI ZA UMMA NA RUSHWA

Dar es Salaam, 15 Desemba 2017
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mhe Dkt. Ashatu Kijaji, amewataka wahitimu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhilrifu wawapo kazini na badala yake wafanye kazi kwa bidii, uadilifu, umakini kwa kuzingatia Sera, sheria, kanuni na taratibu za kitaaluma zilizowekwa.

Dkt. Kijaji aliyasema hayo wakati akiwatunuku vyeti vya kozi mbalimbali wahitimu 3,538 wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania- TIA, wakati wa mahafali ya 15 ya Chuo hicho kwa Kampasi ya Dar es Salaam na Mtwara, Jijini Dar es Salaam.

‘Vitendo vya rushwa na ubadhirifu vina madhara makubwa kwa maisha ya mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa letu kwa ujumla, ni vyema kila wakati mkumbuke kuwa rushwa ni adui wa haki na maendeleo ya Taifa.’ Alieleza Dkt. Kijaji.

Aliwataka Wahitimu wa Taasisi hiyo kujielekeza katika kujiajiri na kuajiri wengine kutokana Soko dogo la ajira hasa ajira rasmi ambalo halikidhi mahitaji ya wahitimu wote nchini.

‘Hatua mliyofikia iwe chachu ya kujiimarisha zaidi kitaaluma ili kuweza kushindana katika soko la ajira na kujiajiri bila kufanya hivyo kazi nyingi za ndani zitachukuliwa na wageni kutoka nje’, alisisitiza Naibu Waziri Kijaji.

Alisema kuwa TIA ni miongoni mwa Taasisi za Elimu ya Juu nchini zinazotoa mafunzo kwa viwango vya kimataifa hivyo ni vyema kuendeleza mafanikio yaliyopatikana bila kusahau kuboresha mahali palipo na mapungufu.

Dkt. Kijaji alisema kuwa fani za Uhasibu ikiwemo Uhasibu wa Fedha za Umma, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa Biashara, Uongozi wa Raslimali Watu na Masoko ni muhimu katika kuendesha uchumi wa viwanda, hivyo umahiri wa wataalamu wanaozalishwa katika taasisi hiyo unatakiwa kuonekana katika kukabiliana na changamoto za usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma, mahitaji ya Soko, ushindani na utandawazi.

Taasisi ya TIA imetakiwa kuendelea kuboresha mitaala ili kukidhi viwango vya kimataifa kwa kuwa Dunia ya sasa ni ya teknolojia hivyo kama Taasisi inatakiwa kuendana na teknolojia hiyo ambayo itasaidia kubadilishana maarifa.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Dkt. Joseph Kihanda alisema kuwa kati ya wahitimu 3,538 wanawake ni 1,846 sawa na asilimia 52.2 na wanaume ni 1,692 sawa na asilimia 47.8. Wahitimu 233 ni wa Kampasi ya Mtwara na wahitimu 3,305 ni wa Kampasi ya Dar es Salaam.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Taasisi hiyo Wakili Said Musendo Chiguma alisema kuwa kwa miaka miwili mfululizo kuanzia mwaka 2015/2016 na 2016/2017 Taasisi hiyo imeongoza kwa kutoa wafaulu wengi wa shahada za juu ya taaluma ya Uhasibu- CPA na taaluma ya Ugavi- CPSP ambapo kwa kipindi cha miaka mitano imetoa asilimia 10 ya wahitimu wote kitaifa.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amewapongeza Wahitimu wote kwa jitihada walizozifanya hadi kufikia hatua hiyo ya kupata vyeti japokuwa amewahimiza kujiendeleza zaidi kitaaluma ili kuongeza weledi.

Imetolewa na:

Benny Mwaipaja

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Fedha na Mipango
15 Desemba 2017

No comments:

Post a Comment

Pages