WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua matengenezo ya
makazi ya muda yanayotarajiwa kutumiwa Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan
pindi atakapohamia Dodoma.
Waziri Mkuu amefanya ukaguzi huo leo mchana (Jumatano,
Desemba 6, 2017) katika eneo la Kilimani, mjini Dodoma ambako yalikuwa makazi
ya Mkuu wa Mkoa huo.
Akitoa taarifa ya ujenzi huo, Waziri wa Nchi (OWM) anayeshughulikia
Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Wenye Ulemavu na Vijana, Bibi Jenista
Mhagama alisema Kikosi kazi cha kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma
kilibaini kuwa mahali alipokuwa akiishi awali siyo sahihi kwa ajili ya makazi
ya kudumu ya Mhe. Makamu wa Rais.
“Pale palikuwa panafaa kwa ajili ya ziara za kikazi
alipokuwa akija Dodoma, kwa hiyo tumeamua tufanye ukarabati hapa, ili aweze kuishi
kwa viwango vinavyostahili.”
Alisema kazi ya matengenezo kwenye makazi yake itagharimu
sh. bilioni 1.5 wakati kazi ya kutenganisha ofisi za watumishi na wasaidizi wa
Makamu wa Rais itagharimu sh. milioni 680.
Waziri Mkuu pia alikagua matengenezo ya Ofisi inayotarajiwa
kutumiwa na Makamu wa Rais ambayo itakuwa eneo la Ndejengwa.
Wakati
huohuo, Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dodoma, Bw.
Steven Simba ambaye anasimamia ujenzi huo, alimweleza Waziri Mkuu wanataraji
kuwa kazi hiyo itakamilika kabla ya Desemba 30, mwaka huu.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S.
L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMATANO,
DESEMBA 6, 2017
No comments:
Post a Comment