WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanasiasa wajiepushe na tabia ya kuingiza
siasa katika suala la kuwaondoa wananchi waishio mabondeni kwa kuwa jambo
hilo linafanywa kwa maslahi ya wananchi wenyewe.
Amesema wananchi wengi wamekuwa wakipoteza
maisha na mali zao kila yanapotokea mafuriko, hivyo ni vizuri kwa viongozi
wakiwemo wabunge washirikiane na Serikali kuwahamasisha wakazi wote wa
mabondeni wahame.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi,
Aprili 19, 2018) wakati akijibu swali la mbunge wa Temeke, Bw. Abdallah
Mtolea katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni
mjini Dodoma.
“Mara
nyingi Serikali imekuwa ikiwataka wakazi ya maeneo ya mabondeni kuhama ila suala hilo limekuwa likikwamishwa na
masuala ya kisiasa. “Wabunge ni mashahidi jambo hili linapoamuliwa, zinaingizwa
siasa.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapa
pole wananchi walioathiriwa na maafa yaliyosababishwa na mafuriko zikiwemo familia
za watu 12 waliofariki mkoani Dar es Salaam.
Katika swali lake, Bw Mtolea alitaka kujua
Serikali ina mpango gani wa kudhibiti madhara ya mvua zinazoendelea kunyesha
mkoani Dar es Salaam.
Mapema akijibu swali la
Mbunge wa Nyang’hwale , Bw. Hussein Nassoro Waziri Mkuu alisema suala la
kurejesha miundombinu iliyoharibika linashughulikiwa na kamati za maafa za mikoa
na wilaya ambazo kwa sasa zinafanya tathmini ili kujua kiwango cha uharibifu na
hatua gani zichukuliwe.
Bw. Nassoro alitaka kujua Serikali
imejipangaje katika kurejesha miundombinu iliyoharibika kutokana na mvua
zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa wito wa wananchi kuhakikisha wanatumia
vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao mbalimbali ya biashara na
chakula. Kuhusu mazao ya biashara amesema Serikali itawasaidia kutafuta masoko.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu
swali la Bi. Aida Khenani (Viti Maalumu), aliyetaka kujua Serikali ina mkakati
gani wa kuandaa masoko ya uhakika kwa mazao ya wakulima.
IMETOLEWA NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S. L.
P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI,
APRILI 19, 2018.
No comments:
Post a Comment