WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ukaguzi unaofanywa kwenye bandari ya
Dar es Salaam kwa wasafiri wanaokwenda Zanzibar, hauna lengo la kuwabagua bali
ni kuimarisha ulinzi wa mipaka ya nchi.
“Hatulengi kuzuia biashara za wafanyabiashara ndogondogo, bali
tunaimarisha ukaguzi ili kuzuia wasafirishaji wa dawa za kulevya, wasambazaji
na wauzaji,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Aprili 19, 2018) Bungeni
mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati
akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Bw. Jaku Hashim Ayoub aliyetaka
kupata kauli ya Serikali juu ya kuwapunguzia makali wafanyabiashara wanaotoka
Zanzibar.
Waziri Mkuu amesema: “Wanaofanya ukaguzi pale bandarini siyo watu wa TRA
peke yao kama Mheshimiwa Jaku alivyosema, bali tukumbuke kuwa Tanzania imeingia
katika vita ya dawa za kulevya, kwa hiyo tunaimarisha ulinzi wa mipaka yetu.”
“Tanzania inapambana na matumizi ya dawa za kulevya, kwa hiyo ukaguzi huu
umelenga kuzuia watumiaji, wasambazaji na wasafirishaji wa dawa hizo. Upekuzi
huu umelenga kupunguza hili tatizo, umelenga abiria wote na siyo Wazanzibari
peke yao,” amesisitiza.
Amesema Serikali inaendelea na mipango ya kutafuta mitambo ya kisasa ya
kukagua mizigo ya wasafiri wanaotumia bandari za Tanzania bara.
Mapema, akiuliza swali lake, Mhe. Jaku alisema: “Kilio cha wabunge wengi
wanaotoka Zanzibar hapa Bungeni ni bandari ya Dar es Salaam kutoza kodi
wafanyabiashara wadogo wanaosafirisha TV au vyerehani. Ni lini utakaa nao au
kufanya ziara ya kushtukiza ili ujionee hali halisi?”
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S.
L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI,
APRILI 19, 2018.
No comments:
Post a Comment