HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 15, 2018

WATANZANIA WATAKIWA KUENDELEZA MATENDO MEMA

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akiteta na Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir katika Baraza la Eid kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoj jijini Dar es salaam Juni 15, 2018. Mheshimiwa Majaliwa alimwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia Baraza la Eid kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Juni 15, 2018. Mheshimiwa  Majaliwa alimwakilisha Rais Dkt John Pombe Magufuli. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Baadhi ya waumini waliohudhuria Baraza la Eid wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati alipohutubia Baraza hilo akimwakilisha  Rais John Magufuli kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Wziri Mkuu).


RAIS Dkt. John Magufuli amewaasa Waislam na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kutenda mema baada ya kuwa wamejisahihisha na kutubu makosa yao ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Hayo yamesemwa leo (Ijumaa, Juni 15, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye amemuwakilisha Rais Dkt. Magufuli kwenye Baraza la Eid El Fitr lililofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Viongozi wanaendelea kuwasihi Waislam wote na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuonesha upendo, umoja na kuvumiliana  hasa baada ya kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Amesema huruma, ukarimu na ucha Mungu ulioneshwa katika kipindi cha mfungo wa ramadhani, uendelee na uwe sehemu ya maisha ya kila siku na kamwe usiwe umeisha baada ya mwandamo wa mwezi wa mfungo mosi.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa upendo, umoja, utulivu, mshikamano na subra uliooneshwa kipindi chote cha mfungo wa ramadhani ni vema ukaendelezwa kwa sababu ucha Mungu si katika mwezi huo pekee.
Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ameniagiza kwa kusema ‘’Waislam ni kielelezo cha taasisi za dini zinazozingatia maadili mema, hivyo wachache wasijipenyeze na kuharibu taswira yao. Ninawahakikishia kuwa Serikali iko tayari kushirikiana taasisi yeyote ya dini ambayo itakuwa tayari kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na taratibu tulizojiwekea nchini’’
Amesema wakati huu wa kusherehekea kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni vema wakakumbuka maneno ya Mtume Muhammad (S.A.W) kwamba ‘’Mwenye kufanya maasi siku ya Eid ni sawa na kumuasi Allah Sub-hanahu Wata’ala siku ya kiyama,’’.
Hivyo amewaasa wananchi wanaposherehekea siku kuu ya Eid El Fitr waendelee kudumisha amani na utulivu kwa kujiepusha na vitendo vibaya vinavyoashiria vurugu, uonevu na uvunjifu wa amani kwa kuwa havina tija.
Awali, Sheikh Mkuu na Mufti waTanzania Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally alitoa wito kwa Masheikh wa Mikoa na Wilaya zote nchini wahakikishe kila wanapofanya mikutano yao mada ya amani na kudumisha uzalendo zisikose kwa kuwa ni vitu muhimu.
‘’Kama mtu huna uzalendo hata dini inapungua, tujenge uzalendo kwa ajili ya kuienzi nchi na kuifanya iendelee kuwa kisiwa cha utulivu. Tuendelee kujenga umoja na mshikamano tusiliache suala hili kwa sababu ndilo liloijenga jamii yetu,’’ alisema.
Pia Mufti Zubeir alisema ni vizuri kwa waislam waunge mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na waache kuishi kwa mazoea. ’’Rais wetu Dkt. Magufuli anafanya kazi kubwa hivyo ni lazima tumuunge mkono na kumpongeza.’’

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, Juni 15, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages