HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

October 21, 2018

Watanzania wang’ara Nagai City International Marathon

Mshindi wa mbio za Nagai City International Marathon kwa wanawake, Angel John, akishangilia na bendera ya Taifa jana. Mbio hizo zilifanyika jijini Nagai Japan. (Na Mpiga Picha Maalum).


NA SALUM MKANDEMBA

WANARIADHA wa Tanzania wameng’ara vilivyo katika Mbio za Kimataifa za Jiji la Nagai nchini Japan (Nagai City International Marathon 2018), baada ya kushika nafasi zote za juu katika Kilomita 42 na 21 (Wanawake na Wanaume).

Tanzania imewakilishwa na wanariadha nane katika Mbio za Nagai City International Marathon, zilizofanyika leo jijini Nagai, Japan, ambako Marco Joseph wa Talent Athletics Club ya Arusha, aliibuka mshindi kwa upande wa wanaume kilomita 42 akitumia saa 2:21:13.

Katika mbio hizo, Marco amefuatiwa na Wilbardo Peter wa klabu ya Polisi, aliyekimbia kwa saa 2:32:12, ambako ukiondoa zawadi, Marco alitwaa Medali ya Fedha, huku Wilbardo akitwaa Medali ya Fedha ya mbio hizo.

Kwa upande wa mbio za kilomita 42 Wanaume, Tanzania pia imeng'ara, baada ya Angelina John Yumba wa Talent Athletics Club kushinda akitumia saa 2:43:21, muda ambao umemuwezesha kufuzu kushiriki Mashindano ya Dunia yatakayofanyika Doha, Qatar mwakani.

Kasi ya Watanzania haikuishia hapo tu, kwani moto wao uliendelea kuunguza wapinzani hadi kwenye nusu marathon km 21 kwa wanaume, ambako Fabiano Nelson Sulle wa klabu ya Polisi, ameshinda akikimbia kwa saa 1:02:53.

Kwa upande wa wanawake km 21, Tanzania iliendelea kutikisa, baada ya nafasi zote nne za juu kubebwa na Watanzania, ambako Amina Mohamed Mgoo ameshinda kwa kutumia saa 1:16:08, akifuatiwa na Rozalia Fabian Duye 1:18:57 (wote wakitokea klabu ya JKT). 

Naye Sylivia Masatu wa Maranatha Athletics Club ya Arusha, ameshika nafasi ya tatu akikimbia kwa muda wa saa 1:32:52, huku Neema Paulo wa Talent Athletics Club, akishika nafasi ya nne kwa muda wa saa 1:41:36.

Msafara huo uliokuwa chini ya Katibu Mkuu wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja, unatarajiwa kurejea nchini Jumatano Oktoba 24.

No comments:

Post a Comment

Pages