WAKATI Tanzania ikielekea kwenye maandalizi ya mbio za dunia
za nyika mwaka huu, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka
amefanikiwa kutimiza ahadi ya kuwalipa wanariadha wote waliokuwa wana madeni
yao kwa shirikisho hilo.
Wanariadha waliolipwa ni pamoja na wasichana sita waliofanya vizuri kwenye mbio za Dunia
za Nyika mwaka 2017 nchini Uganda kiasi cha shilingi milioni 4.8 kwa mgawo wa
shilingi laki nane (800,000) kila mmoja fedha zilizokuwa zimetolewa na
shirikisho la riadha la dunia (IAAF).
Wanariadha hao ni pamoja na Failuna Abdi Matanga, Anjelina
Daniel Tsere, Magdalena Shauri, Sara Ramadhani, Mayselina Mbua, Siata Kalinga
ambao waliibuka washindi wa sita kwa upande wa timu na kuifanya Tanzania
kuzawadiwa kiadi cha dola 6000.
Wengine waliolipwa fedha zao ni wanariadha watatu wa Mbio za
dodoma Marathon mwaka 2016, ambao walikuwa wazawadiwe mabati lakini zilipotea
chini ya mikono ya uongozi wa RT.
Wanariadha Gabriel Geay (kwa upande wa wanaume) na Fadhila
Salum (Kwa upande wa wanawake) waliokuwa washindi wa pili katika mbio zile
alitakiwa kulipwa bati 100 kila mmoja ambapo walifidiwa kiasi cha shilingi
milioni moja kila mmoja (1,000,000) huku
Catherine Lange aliyeshika namba tatu alikuwa anadai bati 40 alipatiwa kiasi cha shilingi 400,000.
“Katika kuelekea
mashindano mapya ya kimataifa, yaliyoko kwenye kalenda ya Shirikisho tumeona
tulipe kwanza madeni yote ya wanariadha waliokuwa wanadai maana naona yanaleta
maneno maneno mengi na yanaweza kuwa sio mazuri kwa afya ya mchezo wa riadha,”
alisema Mtaka
Akitoa sababu za wanariadha kucheleweshewa fedha hizo, Mtaka
alisema kuwa fedha hizo ziliingizwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF)
kwenye akaunti isiyo sahihi ya RT, hivyo walilazimika kutoa taarifa wazirudishe
kwao na watume tena kwenye akaunti sahihi ya shirikisho hali iliyochukua mda
mrefu.
Akipokea fedha hizo mmoja wanariadha hao Anjelina Tsere
alimshukuru Mtaka kwa kutimiza ahadi hiyo ambayo walishaikatia tamaa ya kuipata
tena ambapo amesema hali hiyo imerudisha Imani yao kwa shirikisho na kuahidi
kufanya vema zaidi mwaka huu.
“Kwanza nitumie nafasi hii kukushukuru Rais kwa kutimiza
ahadi hii maana ilitugharimu sana nguvu zetu hivyo kimya cha mda mrefu cha
viongozi wetu ilitufuta kabisa matumaini ya kupata fedha hizi lakini leo
tumepata ni jambo jema na imetutia moyo katika mapambano ya kuelekea mashindano
ya nyika ya dunia tunaahidi tutafanya vema zaidi”
Kwa upande wake kocha mwandamizi wa riadha nchini Zacharia
Barie alisema kuwa hatua ya shirikisho kulipa madeni hayo yatarahisisha kazi za
makocha watakaopata nafasi ya kuwanoa wakiwa kambini na kuwataka wanariadha
kulipa fadhila hiyo waliyotendewa huku wakiiamini shirikisho lao.
No comments:
Post a Comment