Katibu Tawala Mkoa wa Songwe
David Kafulila amesitisha Mkataba wa ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Mkoa na
ya Katibu Tawala Mkoa uliokuwa kati ya yake na Shirika la Ujenzi la Taifa (TBA),
kutokana na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo.
Kafulila akiambatana na
wakuu wa Sehemu wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe amefikia uamuzi huo jana mara
baada ya kutembelea eneo la ujenzi wa nyumba hizo na kukuta hatua ya ujenzi
iliyofikiwa hairidhishi.
Kafulila amesema kasi ya
ujenzi wa nyumba hizo inatia mashaka kutokana na kuwa kazi iliyokwisha fanyika
kwa muda wa siku sitini ni ndogo ukilinganisha kazi na muda uliobakia kufikia
tarehe ya makubaliano ya kukamilika ujenzi.
“Kazi iliyobaki kiuhalisia
haiwezekani TBA wakaikamilisha kwa muda uliobakia, kwani tuliwakabidhi eneo la
ujenzi tarehe 2-2-2019 na tulikubaliana ikifika tarehe 30-06-2019 nyumba hizo
mbili ziwe zimekamilika lakini kwa kipindi cha miezi miwili hakuna kitu wamefanya
na kuna dalili zote za kutokamilisha kwa muda”, ameeleza Kafulila.
Ameongeza kuwa TBA wamekuwa na tabia ya kutekeleza
miradi ya ujenzi kwa kasi ndogo mkoani Songwe na hivyo kusababisha fedha kurudishwa
hazina kuu kutokana na kutozitumia kwa muda unaotakiwa yaani ndani ya mwaka wa
fedha wa serikali ambapo fedha hizo zinakuwa zimetolewa.
“TBA mmekuwa na kawaida ya
kutekeleza miradi yetu kwa kasi ndogo na hivyo kusababisha fedha kurudishwa
hazina, mfano ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wamesababisha takribani Bilioni
3.8 zirudishwe na sasa tunahangaika kuziomba tena, uzembe huu tunaona unelekea
kujirudia tena na sisi kama Mkoa hatuko tayari kila mara tunapewa fedha za
ujenzi halafu zinarudishwa kwa uzembe wa TBA”, ameongeza Kafulila.
Amesema kuwa Mkoa hauna
matatizo na Wizara ya Ujenzi wala shirika hilo la TBA ila lazima hatua za
kusitisha mkataba huo zichuliwe ili kunusuru fedha hizo kurudishwa hazina kuu
kutokana na kuchelewa kuzitumia ndani yam waka wa fedha wa serikali pia ili
nyumba hizo zikamilike kwa muda na kuwezesha makazi ya viongozi.
“Naomba ifahamike mimi na
mkoa kwa ujumla hatuna matatizo na Wizara ya Ujenzi pamoja na TBA lakini
tukilifumbia macho hili hata sisi tutapimwa utimamu wa akili zetu, nimetembelea
eneo la ujenzi zaidi ya mara nne lakini hakuna maendeleo yoyote, kiuhalisia kwa
kasi hii TBA Mtatuangusha, sisi tunapenda kufanya kazi kwa kuendana na kasi ya
Rais wetu”, amesisitiza Kafulila.
Amesema gharama ya Ujenzi
wa Nyumba ya Mkuu wa Mkoa ni shilingi milioni 499.9 na tayari TBA walipewa
malipo ya awali ya shilingi milioni 74.9 huku nyumba ya Katibu Tawala Mkoa
ikiwa na gharama ya shilingi milioni 499.7 na malipo ya awali yaliyotolewa ni
shilingi milioni 74.9
Imeelezwa kuwa TBA hawajawahi
kuwasilisha taarifa ya kazi iliyokwisha fanyika lakini pia hawajaomba fedha
zozote tangu walipwe malipo ya awali huku muda uliobaki ukionyesha kuwa
hataweza kukamilisha kazi iliyobaki.
No comments:
Post a Comment