TUME
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa Julai mwaka huu inatarajia
kuanza zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchini
kwa awamu ya kwanza kwa kutumia teknolojia ya kieletroniki ya
Biometriki.
Teknolojia
hiyo huchukua taarifa za mtu za kibaiolojia na kuzihifadhi katika
kanzidata kwa ajili ya utambuzi na ndio iliyotumika kuandikisha wapiga
kura mwaka 2015.
Hayo
yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume Jaji
Semistocles Kaijage wakati akifungua mkutano mahususi uliyowakutanisha
wahariri wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na maofisa wa NEC kwa
lengo la kujadili kwa pamoja kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la
wapiga kura.
Jaji Kaijage
alisema uboreshaji huo wa daftari la kudumu la wapiga kura utawahusu
wapiga kura wapya ambao ni watanzania waliofikisha umri wa miaka 18 na
zaidi, wapiga kura walipoteza au kadi zao kuharibika, waliohama kutoka
maeneo yao ya awali na kuhamia maeneo mengine ya uchaguzi pamoja na wale
wanaorekebisha taarifa zao.
Alisema
zoezi hilo la uhakiki wa vituo kwa upande wa Tanzania Bara liliongeza
vituo vya kuandikisha wapiga kura kutoka vituo 36,549 hadi 37,407 na kwa
upande wa Tanzania Zanzibar vituo vimeongezeka kutoka 380 hadi 407.
"Maandalizi
mengine yaliyofanyika ni uboreshaji wa majaribio ambao ulilenga kutoa
picha halisi ya uwezo wa vipuli vipya vilivyofungwa katika BVR Kits
ikiwa ni pamoja na mfumo wa uandikishaji wapiga kura ambao utatumika
katika zoezi rasmi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura
litakaloanza hivi karibuni, " alisema.
Alisema
tume iliendesha zoezi la uboreshaji wa majaribio katika kata ya Kihonda
iliyopo halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kata ya Kibuta iliyopo
halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ili kupata mazingira tofauti ya
kijiografia pamoja na idadi ya watu.
"Uboreshaji
huu wa majaribio umefanyika kwa mafanikio ambapo wananchi wengi
walijitokeza, kwa upande wa uwezo wa vipuli na mfumo wa uandikishaji
kumekuwa na mafanikio makubwa hasa upande wa betri za BVR Kits ambazo
zimeonyesha uwezo wa kuhifadhi umeme kwa muda mrefu na hivyo kuweza
kukabiliana na changamoto ya nishati ya umeme katika baadhi ya maeneo
ambayo hayana miundombinu hiyo, " alisema.
Alisema
pamoja na mafanikio hayo kulikuwepo na changamoto mbalimbali ikiwamo ya
wapiga kura kutokuwa na uhakika ama kukumbuka majina yao wanapokwenda
kurekebisha taarifa zao hivyo kutumia muda mrefu kituoni kutafuta majina
yao.
Aidha alisema kwa
mara ya kwanza tume imetoa vibali kwa baadhi ya asasi za kiraia kwa
ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari hilo
la kudumu la wapiga kura.
"Pia
tume imeandaa mwongozo wa utoaji wa elimu hiyo ya mpiga kura ambao
asasi hizo za kiraia zitatakiwa kuufuata wakati wote wa uelimishaji umma
kuhusu uboreshaji wa daftari, " alisema.
Hata
hivyo alisema katika kipindi cha kuelekea uboreshaji huo wa daftari,
vyama vya siasa vimepatiwa orodha ya vituo vya kupigia kura nchi nzima
ili viweze kuweka mawakala katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.
Alisema
tume pia itavishirikisha vyama vya siasa katika eneo la kuteua
watendaji wa uboreshaji vituoni ambao ni waandishi wa vituo, wasaidizi
wa BVR Kits operators ambapo vyama vitapewa orodha ya majina ya
watendaji hao ili vitoe maoni yao.
No comments:
Post a Comment