HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 18, 2019

RC MTAKA NA DHANA YA KUSOMA VITABU

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).


Na Mathias Canal
 
Katika swala la kujifunza katika jamii yetu bado limekuwa ni gumu sana. Ukikutana na watu kumi ukiwauliza unapenda kusoma vitabu utasikia wakisema napenda kusoma vitabu ila sina muda. 

Muda umekuwa kisingizio kwa watu wengi kutupia lawama zao zote katika muda. Watu wanasingizia muda umekuwa tatizo lakini mimi nakataa nasema muda sio tatizo. Habari njema ni kwamba Mungu ametuzawadia zawadi au rasilimali muhimu kuliko zote ambayo ni muda. Kila binadamu aliye hai ana muda wa masaa 24 kwa siku hivyo kwa wiki moja kila mtu ana jumla ya masaa 168 sasa katika masaa 168 kwa wiki nzima unakosa muda kweli wakusoma vitabu na kuongeza maarifa?

Ni hivi karibuni tu wakati wa ziara ya Kikazi katika Wilaya ya Itilima vilevile Wilaya ya Bariadi, Waziri wa Kilimo alizuru kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa biashara ya Pamba ili kumulika madhila wanayopata wananchi kwa kucheleweshewa fedha kutokana na sintofahamu ya wanunuzi kujitokeza kwa wingi katika ununuzi pamoja na wakulima kuwa tayari wamekusanya Pamba kupitia vyama vyao vya Ushirika. Hapa Mhe Japhet Hasunga anakutana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka huku akiwa na vitabu zaidi ya 100 ofisini kwake alivyokwishavisoma katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kama mchambuzi na mdadisi wa mambo nilifanya mazungumzo ya takribani dakika 15 hivi kubaini dhana ya kusoma vitabu, Uongozi na Uwajibikaji. Rc Mtaka anasema “Comrade Mathias akili yako inahitaji maarifa kila siku ili iweze kukua, akili yako inahitaji chakula kila siku kama unavyolisha tumbo lako nalo linahitaji maarifa. Hazina ya akili yako ni maarifa na maarifa yanapatikana katika kusoma vitabu, makala chanya, na siyo kusoma magazeti ya udaku, kusikiliza habari nyepesi nyepesi zisizokuwa na upembuzi yakinifu. 

Jinsi unavyokaa bila kusoma ndivyo akili yako inakaa inazidi kulala ukisoma nayo inazidi kuamka. Jitahidi kusoma na kufikiri kila siku ndio zoezi la akili yako. Kuwa na shahada, astashahada, stashahada, uzamili na uzamivu siyo mwisho wa kusoma au kujifunza bali huo ndio mwanzo wa kujifunza. Usiridhike na maarifa uliyonayo bali kuwa na njaa kali ya maarifa elimu uliyopata darasani ni msingi tu wa kusoma. Mtu anayesoma anakuwa tofauti sana na mtu asiyesoma vitabu tafadhali nakuomba anza kujifunza kuna faida nyingi zisizoelezeka.

Kusoma vitabu sio jambo la lelemama ni jambo la kufanya maamuzi na kutenga muda maalumu kwa ajili hiyo, Lengo kubwa linalowafanya waandishi wa vitabu kuandika vitabu ni kuweka maarifa yao kwenye maandishi, Kwa hakika vitabu huongeza sana uwezo wa kufikiri. Unaposoma vitabu unafahamu mambo ambayo yatakufanya ufikiri zaidi; mara nyingine kitabu kitakuacha na maswali ambayo yatakufanya utafakari kwa kina zaidi juu ya mambo mbalimbali.

Rc Mtaka ni kijana kabisa kiumri ambaye hajavuka hata miaka 40 bila shaka. Anaeleza Maisha yana changamoto mbalimbali; hivyo utahitaji kitu cha kukuhamasisha kutoka hatua moja hadi nyingine. Kwa kusoma vitabu vya hamasa kuhusu maswala mbalimbali ya maisha utaweza kuhamasika zaidi.

Unapotumia muda wako kusoma vitabu, ni wazi kuwa hutopata muda wa kupoteza, Kusoma vitabu kutakufanya utumie muda wako kuongeza maarifa yako zaidi. Tofauti kubwa iliyopo kati ya kusoma vitabu na kuangalia televisheni ni juu ya kuongeza ubunifu wako. Kusoma vitabu hukufanya uondoke katika lindi kubwa la mawazo yanayokutesa na kukutafakarisha juu ya mambo mengine. Waandishi wa vitabu hujenga mazingira ambayo msomaji hujihisi yumo ndani yake.

Dakika mazungumzo yangu na Rc Mtaka ananikumbusha kuwa “Mathias Kadri unavyosoma vitabu vingi kutoka kwa waandishi mbalimbali, ndivyo unavyojitajirisha juu ya misamiati. Kuwa na ukwasi wa misamiati husaidia sana katika maisha ya kila siku. Huongeza kujiamini na uwezo wa kuzungumza mbele ya hadhira. Hadhira yoyote huvutiwa zaidi na mzungumzaji mwenye kujiamini na mwenye uwezo wa kucheza na misamiati ya lugha kwa umaridadi kadri ya muktadha.

Katika ziara hiyo niliondoka Mkoani Simiyu nikiwa na kumbukumbu nzuri na umuhimu wa kukutana na Rc Antony Mtaka nimeamini katika kusoma vitabu Unapata kujua mambo mapya, Ukuaji binafsi wa weledi, kuongeza uelewa, na Kukupa msukumo wa kufanya Maandalizi kabla ya jambo lolote.

Naamini sasa pamoja na mawazo chanya ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe antony Mtaka unakubaliana na mimi kuwa kuna vito vya thamani sana vilivyofichwa kwenye vitabu ambayo watu wengi hawavifahamu.

Ni muhimu ukajijengea utamaduni wa kusoma vitabu mara kwa mara kadri uwezavyo. Unaweza kutumia programu kama vile Balabolka ili kubadili vitabu kuwa sauti na uvisikilize badala ya kuvisoma.

+255756413465

No comments:

Post a Comment

Pages