MASHINDANO ya Riadha ya Uwanjani yajulikanayo kama ‘Mzizima
Track and Field Championship’ yanatarajiwa kufanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam Juni 30 mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chama
cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAAA), Kapteni mstaafu Lucas Nkungu, alisema
mashindano hayo yameandaliwa na kufadhiliwa na Nyange Mtoro ambaye ni Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho.
Nkungu, alisema mashindano hayo lengo lake ni kuibua vipaji na
kuhamasisha mbio za uwanjani, ambako pia Mkoa wa Dar es Salaam utayatumia
kuchagua timu yake itakayoshiriki mashindano ya Taifa yatakayofanyika jijini
Arusha Julai 5 na 6 mwaka huu.
Alisema mashindano hayo yatashirikisha mbio za uwanjani , Kurusha
Tufe, Kutupa Kisahani, Kurusha Mkuki, Miruko Mitatu na Kuruka Chini.
Kapteni mstaafu Nkungu, alisema washindi katika mashindano
hayo watazawadiwa zawadi za fedha taslimu, ambako wa kwanza atapata Sh. 50,000
wa pili 30,000 na wa tatu 20,000 na pia baadhi yao wataingia katika timu ya
Mkoa tayari kwa mashindano ya Taifa.
Alitoa wito kwa klabu, shule na washiriki binafsi kujitokeza
kwa wingi na hakuna ada ya ushiriki.
No comments:
Post a Comment