Mkurugenzi
Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga, akizungumza na watumishi (hawapo
pichani) wakati wa mkutano wake na watumishi wote wa Mamlaka. Wengine katika
picha ni wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi MWAUWASA.
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Watumishi wa Mamlaka ya
Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) wametakiwa kushirikiana
katika utekelezaji wa majukumu yao na kufanya kazi kwa uadilifu.
Mkurugenzi Mtendaji wa
MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga alitoa wito huo hivi karibuni wakati wa
mkutano na wafanyakazi wote uliofanyikia kwenye ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka
kwenye jengo la Maji House ikiwa ni utaratibu aliyojiwekea wa kuzungumza na
watumishi wote kila mwezi.
Mhandisi Sanga alisema ili kupata
matokeo chanya, watumishi wote hawana budi kuhakikisha wanafanya kazi kwa
uadilifu na wanakuwa kitu kimoja na kwamba yampasa kila mtumishi kutambua na
kuheshimu nafasi ya mwenzake kwenye utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
“Hakuna mtumishi aliyebora
kumzidi mwenzake, sote tunahitajiana ili kutimiza majukumu yetu na ndiyo maana
kukawa na mgawanyo wa majukumu. Yatupasa tufanye kazi kwa pamoja kwa kuzingatia
umuhimu wa kila mmoja wetu,” alisema Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga aliwakumbusha
watumishi hao jukumu lao kuu ambalo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya
maji na aliwataka kuhakikisha wanatekeleza jukumu hilo kwa ufanisi na ubunifu mkubwa
ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Alibainisha kwamba endapo
kila mtumishi atatimiza majukumu yake kama inavyostahili, huduma itaboreka zaidi
na maeneo mengi yatafikiwa hasa ikizingatiwa kwamba Jiji la Mwanza linakuwa kwa
kasi.
“Tunapaswa kwenda na kasi ya
ukuaji wa Jiji letu, hatupaswi kuachwa nyuma; kadri Jiji linavyozidi kutanuka
nasi hatuna budi kutanua huduma zetu na busara zaidi ni kufika mbali zaidi kwa
maana yakufika kwenye maeneo ambayo bado Jiji halijafika,” alisema Mhandisi
Sanga.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Edith Mudogo aliwaasa watumishi wote kuwa
wazalendo na aliwataka watumie nafasi walizonazo kuhakikisha wananchi wanapata
huduma ya maji kama inavyostahili.
Alisema MWAUWASA inawatumishi
wa kada mbalimbali na kwamba yampasa kila mtumishi kwa kada yake afikirie namna
bora ya kuhakikisha huduma ya maji inaimarika na kuwafikia wananchi wengi zaidi
hususan wale wa maeneo ya pembezoni.
“Hapa tuna watumishi wa kada
mbalimbali, sasa itapendeza kila mtumishi kwa kada yake atazame ni vipi anaweza
kuwa na mchango wa kusambaza huduma hii ya maji kwa wananchi waishio maeneo ya
pembezoni,” alisema Mudogo.
Aliwahakikishia ushirikiano
kutoka kwa Bodi ya Wakurugenzi hasa ikizingatiwa kwamba dhamira ya Bodi ni
kuona wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya maji bila kujali maeneo waliyopo.
“Sisi kama wajumbe wa Bodi
matamanio yetu ni kuona wananchi wote wa Jiji la Mwanza wanapata huduma ya maji
kutoka MWAUWASA; hatupo tayari kuona mnashindwa kutimiza majukumu yenu, tupo
nanyi, tufanye kazi,” alisisitiza.
Aidha, mkutano huo ulitumika
kutambua jitihada za watumishi waliofanya kazi MWAUWASA kwa miaka 15 ambapo watumishi
sita walikabidhiwa tuzo za utumishi wa muda mrefu ikiwa ni ishara ya kutambua
jitihada zao za muda mrefu katika kuwahudumia wananchi.
Tuzo hizo za utumishi wa muda
mrefu hutolewa kila mwaka ambapo mtumishi anayetimiza miaka 15 hukabidhiwa
ikiwa ni ishara ya kutambua utumishi wake kwa muda wote huo.
No comments:
Post a Comment