Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto
James (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Dkt.
Leonard Chamriho, wakisaini mkataba wa Sh. bilioni 6, kuiwezesha Kampuni ya
Huduma za Meli nchini- MSCL kujiendesha kibiashara, ikiwa ni moja ya mradi wa kimkakati wa kuongeza mapato ya Serikali,
hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini
Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto
James (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt.
Leonard Chamriho, wakionesha mkataba wa Sh. bilioni 6 waliousaini, wa kuiwezesha
Kampuni ya Huduma za Meli nchini- MSCL, kujiendesha kibiashara ikiwa ni moja ya
mradi wa kimkakati
kuongeza mapato ya Serikali
, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa
Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto
James (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila,
wakibadilishana mkataba wa kiasi cha Sh. bilioni 10.7, utakao iwezesha Tume ya
Madini, kuongeza ukusanyaji wa maduhuli
yatokanayo na madini, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha
na Mipango, jijini Dodoma.
Na Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango,
imetoa Sh. billion 10.7, kwa Tume ya Madini nchini na Sh. billion 5.9, kwa
Kampuni ya Huduma za Meli (Marine Service
Company Limited -MSCL) kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya kimkakati, yenye lengo kuongeza mapato yanayotokana
na madini pamoja na kuiwezesha Kampuni ya Huduma za Meli kujiendesha
kibiashara.
Hafla ya utiaji saini mikataba ya fedha hizo umefanyika
Jijini Dodoma kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, ambaye pia ni
Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,
Prof. Simon Msanjila pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamriho.
Bw. James alisema kuwa Sekta ya Madini na Kampuni ya Huduma za Meli, wajifunze kupitia miradi mingine ya kimkakati
katika Halmashauri zilizopewa fedha, ili kuepuka changamoto mbalimbali
zilizojitokeza kwa baadhi ya Halmashauri kushindwa kufikia malengo.
“Fedha hizi sio za bure tutazifuatilia mpaka
shilingi ya mwisho, ili kupata mrejesho wa kuchangia maduhuli katika Mfuko Mkuu
wa Serikali, hivyo fedha hizo zinatakiwa
kutumika kwa ufanisi kwa lengo lililo
kusudiwa”, alisisitiza Bw. James.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango
imeunda kikosi kazi maalum ambacho kitakuwa kinafuatilia maendeleo ya miradi
hiyo na kutoa taarifa Serikalini.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Pro. Simon
Msanjila aliishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha hizo na kuahidi kuwa
watazitendea haki na kuongeza mapato ya Serikali.
"Tumepewa lengo la kukusanya maduhuli ya kiasi
cha shilingi bilioni 475 katika mwaka huu wa fedha 2018/2019, nina kuhakikishia
kuwa lengo hili tutalifikia kwasababu ya uwezeshaji huu wa Serikali na mwitikio
mzuri wa wadau wa sekta ya madini katika kulipa kodi kwa hiari" alisema
Prof. Msanjila
Alisema kuwa Sekta ya madini ni muhimu kwa
maendeleo ya uchumi wa nchi, uwezeshaji huo utawezesha kutatua changamoto
mbalimbali zilizokuwa zikiikumba Tume ya Madini kwa lengo la kuongeza
ukusanyaji wa mapato yanayotokana na madini.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula, alisema
kuwa uwezeshaji huo utaiwezesha Tume hiyo kufikia lengo na kuahidi kuendelea na
juhudi za kuhakikisha maduka ya madini nchini yanaboreshwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamriho, aliishukuru Serikali kwa
kuipatia Kampuni ya Meli nchini (MSCL) kiasi cha shilingi bilioni 5.9
zitakazotumika kukarabati baadhi ya meli zilizopo pamoja na kuweka mifumo ya
kieletroniki ya kukusanya maduhuli ya Serikali.
Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za
Meli, Bw. Eric Hamissi, aliahidi Serikali kuwa hawatoiangusha na kubainisha
kuwa kampuni hiyo ni ya kimkakati na inaweza kuchangia uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment